Tumia muda huu kusuluhisha masuala kati yako na mpenzi wako.

Iwapo unapitia wakati mgumu ukiwa nyumbani haswa kwa kuwa uhusiano wako na mpenzi wako unayumbayumba,  basi mshauri Moffat Kago anakutaka utumie muda huu kutatua masuala ambayo yamejirundika kwa muda, ili ufanye nyumba yako kuwa na mzingira mazuri tena.

Hayo yakijiri, siku kuu ya pasaka imewadia lakini wakati huu hatutakongamana kuisherehekea kutokana na janga la coronavirus. Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka anakuomba kuisherehekea siku kuu hii ukiwa nyumbani, ukiwaombea walioathirika.

Kwingineko, taasisi ya utafiti wa kimatibabu nchini, KEMRI, imesitisha utafiti wa mzigo wa virusi vya HIV ili kuangazia vipimo vya coronavirus.

Taasisi hiyo inahitajika kufanya vipimo vya sampuli elfu 35 za coronavirus kila siku. Mkuu wa maabara Matilu Mwau anasema hatua hii itadumu hadi baadae mwezi  huu, lakini inaweza kuongezwa muda.

Wanaume 107 ni miongoni mwa waathiriwa 184 wa virusi vya corona ambao wamethibitishwa humu nchini. Wanawake 77 na watoto watatu chini ya umri wa miaka 15 ni miongoni mwa waathiriwa hao.