Ubabe wa kisiasa baina ya Ruto na Raila watawanya wanasiasa wa kike

Wabunge wa kike wamegawanyika huku wengine wakivuta upande wa Naibu Rais William Ruto na wengine wakimuunga mkono kinara wa upinzani Raila Odinga.

Mgawanyiko huo umepelekea kubuniwa kwa mirengo miwili, mmoja wa Kieleweke na mrengo mwingine ukivuta kamba upande wa Tangatanga.  Kundi moja la wanawake linaloegemea upande wa kieleweke linawaunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa Nasa Raila Odinga kupitia vuguvugu la Embrace.

Kundi lingine la wanawake linatifua kivumbi cha kisiasa kwa kuegemea upande wa Tangatanga unaopigia debe azma ya urais ya naibu rais William Ruto kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.  Pande hizo mbili zimekuwa zikilumbana huku uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 ukikaribia.

Makundi haya yameanzisha ziara katika maeneo mbali nchini kupigia debe vinara wao hali ambayo inatishia kuongeza joto katika tanuri la kisiasa nchini miezi 34 kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Gazeti la The Star limebaini kuwa makundi hayo yanapanga kuanzisha mikakati ya kutafuta pesa ili kupiga jeki mipango na ratba zao.

Kuna madai kwamba kundi la kieleweke linapokea ufadhili kutoka kwa baadhi ya maafisa wa serikali wanaopinga azma ya arais ya Ruto. Kundi hilo la linalojiita Embrace, linaongoza na wabunge wakike wenye ushawishi kutoka Jubilee na upinzani. Lengo ni kudidimiza uungwaji mkono wa naibu rais miongoni mwa kinamama kote nchini.

Mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Nairobi Esther Passaris na mwenzake wa Homa Bay Gladys Wanga ni miongoni mwa wanaounga mkono mikakati ya Embrace. Kundi hilo pia linaungwa mkono na Katibu msimamizi katika wizara ya utumishi wa umma Rachel Shebesh, huku uvumi ukizuka kwamba kundi hilo linapata ufadhili kutoka kwa ofisi ya rais.

Kundi linalomuunga mkono naibu rais linaongozwa na mwakilishi wa wawanake wa Kirinyaga Purity Ngirici, Seneta maalum Millicent Omanga na mbunge wa Kandara Alice Wahome. Kundi hilo linalenga kuanzisha miradi ya kuimarisha hali za kinamama kiuchumi mashinani ili kukabili umaarufu wa kundi la Embrace.

Taarifa ya James Mbaka