Uchaguzi Wa Ndani Wa ODM Kuendeshwa Na IEBC - Nyong'o

Anyang-Nyongo
Anyang-Nyongo
Seneta wa kaunti ya Kisumu Prof. Anyang Nyong’o ameunga mkono hatua ya kushirikishwa kwa tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC kuandaa chaguzi za ndani ya chama cha ODM.
 
Kulingana na Nyong’o, uwazi na uhuru katika zoezi la chaguzi za chama cha ODM utafanikishwa na kuendeshwa kwa zoezi hilo na tume ya IEBC.

 Nyong’o amesema chama cha ODM kilitazamia kutumia tume ya IEBC kwenye chaguzi zake za mwaka 2013 ila ombi lao lilikataliwa.
 
Amehoji kuwa hakuna kinachozuia IEBC kuendesha chaguzi za chama hicho kwa maana tume hiyo imefanikisha chaguzi za taasisi mbali mbali nchini.
 
Seneta huyu ameyasema haya akiwa katika kanisa la Arina AIC wakati wa hafla ya kuchangisha fedha wa minajili ya kanisa hilo.

Ameongeza kuwa tume hiyo ya uchaguzi inalenga kufanyiwa marekebisho ambayo yataboresha tume hiyo na hivyo itaweza kuandaa chaguzi za vyama kwa utaratibu bora.

Hayo yakijiri, Seneta mteule Joy Gwendo ni kiongozi wa hivi punde kuunga mkono hatua ya kutumiwa kwa tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka IEBC kuandaa chaguzi za ndani ya vyama vya kisiasa nchini.

 
Akizungumza akiwa Kisumu Mashariki, Gwendo amesema hatua hii itasaidia pakubwa kwa taifa hili kuandaa chaguzi zitakazozingatia haki na zenye uwazi.
 
Hata hivyo, Gwendo amependekeza kutolewa kwa mafunzo kwa maafisa wapya wa tume ya IEBC ambao watachukua  nafasi zitakazoachwa wazi ili kuwasaidia kuendesha chaguzi za vyama kwa mujibu wa sheria.