Uhuru ahakikishia kila mtoto elimu ya msingi

Serikali itasalia imara katika juhudi zake kuhakikisha watoto wote wa Kenya wanapata elimu ya msingi.

Rais Uhuru Kenyatta aliyezungumza katika Ikulu ya Nairobi alipokabidhi basi lenye uwezo wa kubeba abiria 52 kwa shule ya upili ya wasichana ya Kamacharia kutoka kaunti ya Murang'a, alisema Serikali yake itaendelea kuekeza katika upanuzi wa miundomsingi ya shule kuhakikisha watoto wote wa Kenya wanapata elimu.

Ili kuonyesha umuhimu wa juhudi za Serikali na wazazi wao, Kiongozi wa taifa alitoa changamoto kwa wanafunzi kote nchini kutia bidii katika masomo yao kwa kuepuka vizuizi vinavyohusishwa na juhudi potovu za kujifurahisha kwa muda ikiwemo uhusiano wa kimapenzi.

“Tia bidii, kuweni wakakamavu. Mnayo safari ndefu. Tusiwe na haraka, hakuna haja ya kuwa na haraka, lengeni masomo yenu,” kasema Rais.

Rais aliwakumbusha wanafunzi hao kwamba vifaa vya shule na miundomsingi inayotelewa na Serikali vinalenga kuhakikisha hawatenganishwi na malengo yao muhimu ya kuimarika kwenye masomo yao.

“Bila shaka hatua hii ni ya kuwahimiza muendelee na masomo yenu, pia mnahitaji kufanya bidii. Kwa msaada huu itakuwa vyema kwenu kutuletea matokeo bora mwishoni mwa mwaka,” Rais Kenyatta kawaambia wanafunzi wa shule ya wasichana ya Kamacharia.