Ulemavu usiwe kikwazo kwa ufanisi wako

Na Sairin Lupia

Deisemba tarehe tatu kila mwaka huwa siku ya walemavu duniani. Kufikia sasa hatua muhimu zimepigwa katika kuimarisha maisha ya walemavu ili waishi maisha sawa na watu wengine katika jamii licha ya hali zao. Serikali imebuni sera mbali mbali za kuwakinga watu wanaoishi na ulemavu.

Ni kupitia sera hizi ambapo kuna nafasi maalum katika seneti, bunge la kitaifa na mabunge ya kaunti zilizotengewa tu watu wenye ulemavu. Katika seneti kwa mfano kuna seneta maalum Isaac Mwaura na katika mbunge kuna mbunge maalum David Ole Sangok ambao ni moja wapo tu wa walioteuliwa kuwakilisha maslahi ya walemavu.

Watu wanaoishi na ulemavu hukumbana na changamoto nyingi katika maisha, vijana wenye ulemavu hawajasazwa wao vile vile wana matatizo katika maisha yao ya kila siku. Nchini Kenya idadi ya vijana walemavu inazidi kuongezeka kila siku, wengi wakizaliwa na ulemavu huku baadhi yao wakijipata katika hali hii kutokana na ajali au maradhi. Kuna changamoto chungu nzima zinazowakumba vijana walemavu, kutoka kwa ukosefu wa vyuo vya elimu vya kutosha kukidhi mahitaji yao hadi kwa ukosefu wa ajira kwa sababu waajiri wengi hawako tayari kuwapa walemavu nafasi.

Habari zaidi;

Nilipokuwa katika shule ya upili, nilikuwa na rafiki wa karibu aliyekuwa mlemavu na alipitia hali ngumu sana shuleni. Katika nyingi ya taasisi zetu za masomo hakuna mazingira mahsusi inayowafaa walemavu. Rafiki yangu alikuwa akilazimika kupanda ngazi kila siku ili ahudhuriye masomo katika madarasa yaliokuwa juu kwa ghorofa. Sio tu katika shule za upili hata vyuo vikuu bado vipo nyuma katika kubuni mazingira bora ya watu wenye ulemavu.

Mbali na uhaba wa taasisi za elimu kwa walemavu walimu waliohitimu kuwafunza watu wenye mahitaji maalum ni wachache pia.  Kutokana na maumbile yao watu hawa wanahitaji kushughulikiwa kwa njia spesheli hasa katika masomo ili waweze kufanikiwa kama watu wengine. Wanafaa pia kupewa fursa sawa katika jamii ili kuonyesha uwezo wao katika nyanja mbali mbali.

Habari zaidi;

Baada ya kutia bidii masomoni na kujiunga na vyuo vikuu, wengi wao hukata tamaa kwani hakuna mikakati maalum katika vyuo vingi kufanikisha uwepo wao au mahitaji yao maalum. Walemavu wengi wamelazimika kutupa ndoto zao katika kaburi la sahau licha ya kutamani sana kuwa madaktari au hata wahindisi kwa kukosa taasisi maalum za kuwawezesha kufanikisha ndoto hizo.

Je, wajua kwamba hakuna chuo kikuu maalum cha walemavu nchini Kenya?, wengi wao hupata alama nzuri katika shule spesheli za walemavu na kuitwa kujiunga na vyuo vikuu lakini hulazimika kukatiza masomo yao kutokana na kutokuwepo kwa vyuo vikuu spesheli kushughulikia matakwa yao maalum.  Hii ndiyo sababu idadi ya walemavu katika vyuo vyetu ni ya chini mno, jambo ambalo linasikitisha sana. Hali hii inawafanya walemavu wengi kusitisha masomo yao baada ya kumaliza shule za upili.

Habari zaidi;

Ni jukumu la serikali kuwapa walemavu nafasi sawa na wenzao wasio walemavu. Idara husika sinafaa kufanya ukaguzi ili kubaini kama mijengo katika taasisi za masomo inazingatia kanuni zilizowekwa na serikali kwa minajili ya watu wenye mahitaji maalum.

Wakati umewadia kwa washikadau katika sekta ya elimu waje pamoja ili kuweka mikakati ya kufanikisha elimu ya walemavu. Kila mtu anapaswa kupewa fursa sawa kujiendeleza kimasomo na kimaisha. Ulemavu sio udhaifu na hakuna mtu anayepaswa kuacha ndoto zake kwa sababu ya aina yoyote ya ulemavu. Sote tuko sawa.

Mwandishi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi.