Akizungumza na gazeti la The Star siku ya Jumatatu, Profesa Atwoli Lukoye amesema kutorundikana kwa watu, kutumiwa kwa maski na kunawa mikono kila mara bado ndio njia muhimu sana za kujikinga dhidi ya virusi vya corona.
Hii ni baada ya kundi la wanasayansi 239 kutoka mataifa 32 kuliandikia barua shirika la afya duniani WHO na kulipa ushahidi huo mpya wakieleza kwamba matone madogo madogo ya hewa yanaweza kuwaambukiza watu ugonjwa huo.
Wamesema kuna uwezekano wa maambukizi hata ndani ya majumba, katika sehemu zenye watu wengi, sehemu zisizokuwa na hewa safi na nyakati mtu havalii maski kwa muda mrefu.
Wanalitaka shirika la WHO kurekebisha mwongozo wake wa jinsi ya kukabiliana na virusi hivyo baada ya kugunduliwa kwamba matone ya hewa yana uwezo wa kuwezesha usambaaji wa virusi vya corona.
WHO imekuwa ikishikilia kwamba virusi hivyo husambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia matone ya mdomoni au puani ambayo hutolewa wakati mtu anapokohoa au kupiga chafya au akizungumza
Lakini Atwoli amesema huenda kuna tofauti adimu sana kati ya matone yalio hewani na matone ya kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine.