Gidi aanza kujifunza Kifaransa baada ya kuchekwa na binti yake kwa lafudhi mbaya

Gidi ameanza jaribio la nne la kujifunza Kifaransa baada ya kufeli katika majaribio matatu ya awali.

Muhtasari

•Mtangazaji huyo alieleza matumaini yake kuwa mara hii hatimaye atafanikiwa kusoma lugha hiyo ya kigeni.

•Gidi alisema anakusudia kumshangaza bintiye kwa ubabe wake wa Kifaransa katika muda wa miezi michache ijayo.

Gidi na bintiye Marie-Rose
Image: INSTAGRAM// GIDI OGIDI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Ogidi ameanzisha jaribio lake la nne la kujifunza lugha ya Kifaransa baada ya kushindwa katika majaribio yake matatu ya awali.

Mnamo siku ya Jumatatu, mtangazaji huyo mzoefu alitangaza kwamba angeanza masomo yake jioni hiyo.

Gidi alieleza matumaini yake kuwa mara hii hatimaye atafanikiwa kusoma lugha hiyo ya kigeni.

"Hili litakuwa jaribio langu la 4 lakini safari hii nina matumaini kuwa nitafanikiwa," alisema kupitia mtandao wa Instagram.

Mtangazaji huyo mahiri alifichua kuwa safari yake ya nne ya kujifunza Kifaransa ilianza baada ya kuchapisha video ya binti yake, Marie-Rose, akijaribu kumfundisha lugha hiyo takriban  miezi miwili iliyopita.

"Watu wengi walionitakia heri nchini Ufaransa na Kenya walijitolea kunisaidia kujifunza Kifaransa. Hatimaye nilifuatiliwa kupitia Ubalozi wa Ufaransa na Alliance Francaise ambao wametoa mpango wa ushirikiano kujifunza Kifaransa," alisema.

Katika video iliyochapishwa mwezi Januari, Marie-Rose alionekana akimfundisha baba yake maneno ya Kifaransa. Rose alicheka sana lafudhi ya baba yake alipokuwa akijaribu kurudia maneno ya Kifaransa baada yake.

Gidi alifichua kuwa anakusudia kumshangaza binti huyo wake mdogo kwa ubabe wake wa Kifaransa katika muda wa miezi michache ijayo baada ya kuanza masomo katika Alliance Francaise siku ya Jumatatu.

"Nimekuwa nikijaribu kuja hapa kuanza masomo yangu kisha ninaacha. Nina matumaini kwamba wakati huu nitafanya vyema," alisema.

Binti mdogo wa Gidi, Marie- Rose anaishi na mama yake nchini Ufaransa na mtangazaji huyo huwatembelea mara kwa mara anapopata mapumziko kutoka kazini. Wawili hao wanaonekana wazi kuwa na uhusiano mzuri wa baba na binti na aghalabu huwa na furaha kila mara wanapopata nafasi ya kuwa pamoja.