Ghost Mulee afunguka kuhusu manufaa ya kufanya kazi na Gidi katika miaka 15 iliyopita

Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alitaja miaka yake mingi kwenye redio kuwa iliyojaa tajriba ya kushangaza.

Muhtasari

•Jacob ‘Ghost’ Mulee ameadhimisha muongo mmoja na nusu redioni huku ulimwengu mzima ukiadhimisha Siku ya Redio Duniani.

•Pia hakusahau kuwatambua mamilioni ya mashabiki wao akisema, "Siku njema ya Redio Ulimwenguni na asante kwa kusikiliza."

Image: RADIO JAMBO

Mtangazaji mwenza wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob ‘Ghost’ Mulee ameadhimisha muongo mmoja na nusu redioni huku ulimwengu mzima ukiadhimisha Siku ya Redio Duniani.

Katika chapisho la Jumanne asubuhi, kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alitaja miaka yake mingi kwenye redio kuwa iliyojaa tajriba ya kushangaza.

Mtangazaji huyo mcheshi pia alichukua fursa hiyo kusherehekea kufanya kazi pamoja na mtangazaji mwenzake, Joseph Gidi almaarufu Gidi Gidi akisema kuwa kufanya kazi naye kumefanya tajriba hiyo kuwa bora zaidi.

"Kuwa katika Redio kwa miaka 15 imekuwa uzoefu kamili wa maisha. Kufanya kazi na Gidi kumeleta furaha, uvumilivu, subira na vicheko vingi,” Ghost alisema kupitia mtandao wa Instagram.

Pia hakusahau kuwatambua mamilioni ya mashabiki wao akisema, "Siku njema ya Redio Ulimwenguni na asante kwa kusikiliza."

Mapema siku ya Jumannne, Gidi alikuwa amechukua muda kusherehekea ushirikiano wake na mtangazaji mwenzake Jacob ‘Ghost’ Mulee.

Katika chapisho kwenye mitandao yake ya kijamii, mwanamuziki huyo wa zamani alibainisha kuwa ushirikiano wa utangazaji wa redio ni kama ndoa akidokeza kwamba watangazaji wenza wanapaswa kufahamiana na kukabiliana na kila mmoja, jambo ambalo yeye na Ghost wamefanikiwa kufanya vizuri kwa zaidi ya muongo mmoja na nusu.

"Ushirikiano wa utangazaji wa redio ni kama ndoa, huwezi kutoboa ikiwa huwezi kukabiliana na ujinga wa kila mmoja!," Gidi Ogidi alisema kupitia mtandao wa Facebook.

Aliambatanisha taarifa yake na picha nzuri zake na Ghost wakiwa studio.

"Imekuwa miaka 16 ya redio ya asubuhi na rafiki yangu Ghost Mulee," aliongeza.

Mtangazaji huyo mahiri wa redio pia alichukua fursa hiyo kuwatambua mamillioni ya mashabiki wao na kuwathamini kwa sapoti yao inayoendelea.

“Asanteni kwa mashabiki wetu wote kwa kusikiliza. Heri ya Siku ya Redio Duniani,” aliandika.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na mwanahabari Samuel Maina, Ghost Mulee alifichua kuwa asingekuwa mtangazaji wa Redio, basi angekuwa anafanya kazi inahusiana na kuwashughulikia wanyama/

“Kama nisingekuwa Mtangazaji wa Redio, ningekuwa KDF ama ningekuwa KWS. Ningekuwa mtu nashughulika na wanyama," alisema.