Sikuwahi kuangalia umri wa Guardian Angel, ilinichukua muda kujua miaka yake- Esther Musila

Muhtasari

•Musila ,52, alidai kwamba alimuona Guardian Angel kuwa mtu aliyekomaa sana walipokutana na kujuana.

•Guardian Angel alidai kwamba hakuwahi kujali kuhusu pengo kubwa kati ya umri wake na Bi Musila.

•Wanandoa hao walifichua kuwa walichumbiana kwa chini ya kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kuanza kuishi pamoja. 


Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Bi Esther Musila amekiri kwamba ilimchukua muda mrefu kujua umri halisi wa mume wake Guardian Angel.

Akiwa kwenye mahojiano na Massawe Japanni katika kitengo cha Ilikuaje?, Musila alisema hakuzingatia umri wa mwanamuziki huyo walipokutana kwa mara ya kwanza.

Mama huyo wa watoto watatu mwenye umri wa miaka 52 alidai kwamba alimuona Guardian Angel kuwa mtu aliyekomaa sana walipokutana na kujuana.

"Sikuangalia umri wake. Ilinichukua muda kujua umri wake. Haikuwa kuhusu umri wake. Nilipendezwa na jinsi alivyokomaa. Yeye ni mtu aliyekomaa sana," Musila alisema.

Kwa sasa Guardian Angel ana umri wa miaka 35.

Wanandoa hao walifichua kuwa waliungana vizuri tangu siku ya kwanza walipokutana, ambayo ilikuwa Machi 13, 2020. Walifichua kuwa walichumbiana kwa chini ya kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kuanza kuishi pamoja. 

Musila aligura kwake na kuhamia kwa mwanamuziki huyo baada yao kujitosa kwenye mahusiano ya kimapenzi.

"Nilihama. Bado niko na kwangu kwa sababu watoto wangu bado wanaishi pale lakini nilipanga nusu ya nguo zangu na kuhamia kwake," Musila alisema.

Alisema kwamba alihofia kupokea kejeli kutoka kwa Wakenya baada ya habari za mahusiano yake na Guardian kufichuka.

"Nilikuwa natoka kwa maisha ya siri na kuingia maisha ya umaarufu, umri wangu ndio ulikuwa shida. Nilihofia watu wangesema nini," Alisema.

Guardian Angel kwa upande wake alidai kuwa hakuwahi kujali kuhusu pengo kubwa kati ya umri wake na Bi Musila.

Wapenzi hao wamechumbiana kwa zaidi ya miaka miwili. Wawili hao walifunga pingu za maisha Januari mwaka huu.

Angel ameweka wazi kuwa anafurahia ndoa yake na Musila licha ya kejeli nyingi wanazopokea kwenye mitandao ya kijamii.

"Kama hivi ndio kuwekwa inaonja, wacha niwekwe milele. Kama hivi ndio kuwekwa iko, ni tamu," Angel aliwajibu wanaodai kuwa yeye ni Ben 10 wa mkewe.

Aidha aliweka wazi kuwa yeye ndiye kiongozi wa boma yao huku akifichua kuwa hajawahi kuishi kwa nyumba ya mkewe.