Mercy Tarus aeleza walivyojua wametapeliwa katika programu ya masomo ya Canada, Finland

Mercy alisema walikuwa wameahidiwa wangeondoka Kenya kabla ya Desemba mwaka jana lakini miezi 8 baadaye bado wako hapa.

Muhtasari

•Mercy alifichua kuwa walianza kushuku kuwa  wamechezewa baada ya safari yao kuendelea kuahirishwa huku wapangaji wakiendelea kuwadai pesa zaidi.

•Alisema kuna wanafunzi wapatao 321 ambao bado hawajasafiri kwenda Finland na Canada licha ya kuwa wamelipia masomo hayo.

katika studio za Radio Jambo mnamo Agosti 14, 2023.
Mercy Tarus katika studio za Radio Jambo mnamo Agosti 14, 2023.
Image: RADIO JAMBO

Mercy Tarus, mwanadada ambaye amekuwa akivuma katika wiki moja iliyopita baada ya video yake akiwazomea hadharani viongozi wa kaunti ya Uasin Gishu kusambaa kwenye mitandao ya kijamii amejitokeza na kueleza jinsi walikuja kubaini kuwa wametapeliwa.

Katika mahojiano na Massawe Japanni kwenye Radio Jambo, msusi huyo alifichua kuwa walianza kushuku wamechezewa baada ya safari yao kuendelea kuahirishwa huku wapangaji wakiendelea kuwadai pesa zaidi.

Mercy alidokeza kuwa awali walikuwa wameahidiwa kuwa wangesafiri ifikapo Desemba mwaka jana baada ya kukamilisha taratibu zote za usafiri lakini kuahirishwa kwa mambo kuliwafanya kungoja kwa muda mrefu.

“Sisi tuliambiwa Disemba haingefika kama bado mko hapa. Tukalipa pesa haraka, tulikuwa tunaangalia siku zetu za usoni tunaona ni nzuri. Tulipolipa wakatuambia itabidi tuende medical, tufanyiwe biometrics na mambo mengine. Mimi nilingoja hadi Desemba 7 mwaka jana nikaenda medical ambayo ilikuwa shilingi 36,000 na hazikuwa zimehesabiwa kwa pesa tulikuwa tumetoa. Tulitoa zaidi ya milioni moja. Bado tulikuwa tunatoa pesa, kuna pesa ya nauli na utalala wapi, utakula wapi. Tulipoenda medicals Disemba tuliambiwa tungoje kiasi kwa sababu bado hatujaenda biometrics, tukaambiwa Februari haipiti kama tuko Kenya ,” Mercy alisimulia.

Mhitimu huyo wa chuo kikuu alieleza kwamba walikuwa wakiwasiliana na maafisa katika afisi ya Michezo, Vijana na Burudani ya kaunti ya Uasin Gishu ambao waliwapa taarifa kuhusu maendeleo.

Maafisa hao hata hivyo waliendelea kuchelewesha siku yao kuondoka Kenya na kuwapa sababu tofauti za kuahirishwa.

“Baada ya kuambiwa stori za Februari, nilienda Biometrics mnamo Januari 26. Walisema hiyo ndiyo siku walikuwa wanazindua Visa, tukaambiwa tuache pasipoti zetu. Februari ilipita kama hatujaenda. Nilifaa kuanza masomo tarehe 1 Mei kwa sababu tulikuwa tumeahirisha sana. Shule ikatuambia tumepatiwa wiki mbili tuwe tumefika shule na kama bado hatutakuwa tumeenda watajua cha kufanya. Hatukuenda juu bado tu hapa,” alieleza.

Aliongeza “Baada ya Mei 1 tukaambiwa tungoje Septemba tukaona sasa wanatufanyia vile walifanyia wasee wa Finland. Tuliona sasa hapa ni uongo kwa sababu hawawezi kuwa wanatuambia kila siku tungoje miezi miwili, wiki mbili. Tuliitwa mkutano fulani Juni 15 tukaambiwa sasa tuongeze pesa kwa sababu kumekuwa na changamoto. Walisema ile 600k tulitoa sio 60% bali ni 50%. Walisema sasa wamekuja kutufafanulia. Walisema tuongeze 600k ingine juu ya ile 600k tulikuwa tumelipa.

“Tukaulizia sana pesa ya makazi wakasema ile tulikuwa tumelipa hawawezi kufuatilia kwa sababu pesa ilikuwa benki ni kidogo, ilikua 1.8m. Tuliambiwa sasa tuongeze 400k . Nauli ya ndege bado hatujaweka. Hiyo ni milioni moja tayari. Ongeza 600k, ongeza 400k, ongeza 180k ya ndege, 100k ya gharama alafu tukaambiwa sasa utaenda."

Kulingana na Mercy, ni wachache tu kati yao waliokubali kulipa pesa za ziada walizodaiwa ambazo zilifanya jumla ya pesa zilizotolewa kwa programu hiyo ya masomo ya ng'ambo kuongezeka hadi zaidi ya shilingi milioni 2.

Alisema kuna wanafunzi wapatao 321 ambao bado hawajasafiri kwenda Finland na Canada licha ya kuwa wamelipia masomo hayo ilhali takribani 278 walikwenda mwaka jana na wengine 44 walisafiri mwaka huu.