Yesu wa Tongaren azungumzia elimu yake, akana kunywa busaa "Nalewa divai ya Mbinguni"

Bw Simiyu alifichua kwamba hakwenda mbali na masomo yake.

Muhtasari

•Yesu wa Tongaren alifichua kwamba alifaulu tu kusoma hadi kidato cha kwanza na baada ya hapo hakuweza kuendelea.

•Massawe alimshauri Yesu wa Tongaren apunguze unywaji wa Busaa ili kuepuka kulazwa tena hospitali.

Yesu wa Bungoma azungumzia kusulubishwa pasaka
Yesu wa Bungoma azungumzia kusulubishwa pasaka
Image: Maktaba

Kwenye kipindi cha Bustani la Massawe siku ya Alhamisi, Bw Eliud Simiyu almaarufu Yesu wa Tongaren alishiriki mahojiano ya simu na mtangazaji Massawe Japanni ambapo alifunguka kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maisha yake.

Katika mahojiano hayo, Bw Simiyu alifichua kwamba hakwenda mbali na masomo yake. 

Mzee huyo kutoka Bungoma anayedai kuwa yeye ni Yesu Kristo ambaye amerudi duniani kwa mara ya pili  ili kuwakomboa Walimwengu alibainisha kuwa Biblia haisemi kuhusu historia ya masomo ya Yesu.

"Kwa Biblia mliona wapi historia ya Yesu ya kusoma?"  Simiyu alihoji alipoulizwa kuhusu kiwango cha masomo yake.

Baba huyo wa watoto wanane alifichua kwamba alifaulu tu kusoma hadi kidato cha kwanza na baada ya hapo hakuweza kuendelea.

Simiyu alisema licha ya kutosoma sana alifanikiwa kupata kazi maalum ya kuwakomboa walimwengu ambayo anaifurahia.

"Mimi sikusoma masomo ya ulimwengu sana. Nilifika katika darasa la nane. Nilijiunga na shule ya upili lakini nikabaki kidato cha kwanza. Namshukuru Mungu kwa hii kazi yangu," alisema.

Licha ya kutokuwa na elimu kubwa, Bw Simiyu alibainisha kuwa ameweza kutembelea mataifa yote duniani kiroho.

"Saa hii nimezunguka mataifa yote ya dunia kiroho na hata walimwengu wananitazama sasa kwenye runinga," alisema.

Alifichua kuwa alizindua kanisa lake 'Kanisa la Yesu' mwaka wa 2009 na ameendeleza  injili kwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita. Alisema kuwa kanisa lake lina manabii kumi na wawili pamoja na washirika wengine.

Katika mahojiano hayo, mtangazaji Massawe alimshauri Bw Simiyu apunguze unywaji wa Busaa ili kuepuka kulazwa tena hospitali.

Yesu wa Tongaren hata hivyo alionekana kujitenga na madai ya kubugia kileo hicho na kusema, "Nalewa divai ya Mbinguni ya Baba."

Bw Simiyu alipoulizwa ikiwa watoto wake hujitambulisha kama wana wa Yesu shuleni, aliweka wazi kwamba huwa wanatumia jina la ukoo 'Simiyu'.

Wasikilizaji wengi waliopiga simu studioni kutoa maoni kuhusu Yesu wa Tongaren hata hivyo walionekana kumpuuza wakimtaja kama mwenye mzaha tu.