Patanisho: Mwanadada agura ndoa baada ya mumewe kupendekeza wapate mtoto wa pili

Muhtasari

•Koech alidaiu alitaka kupata mtoto wa pili mwaka huu juu alikuwa na wasiwasi kwani hapo awali mkewe alikuwa amemtahadharisha ifikapo 2023 hangekubali kupata mtoto mwingine.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Simon Koech (25) kutoka Eldoret alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake  Joan (24).

Koech alisema ndoa yao ya miaka mitatu ilisambaratika mwezi Septemba wakati alisihi mke wake wapate mtoto wa pili.

Alisema mkewe alimwambia asubiri hadi mwaka wa 2025 wakati ambapo angefanya maamuzi iwapo angekubali kupata mtoto mwingine.

"Aliniambia mpaka 2025. Huyo mwingine saa hii ako na miaka mitatu.Hiyo ni mbali sana, nataka niharakishe lakini anakata. Tulikuwa kwa ndoa miaka mitatu. Tulikuwa tunapanga kupeleka mahari mwezi wa nne mwaka ujao. Nilikuwa nampenda sana kwa roho yangu yote" Alisema Koech.

Alieleza kwamba amekuwa akijaribu kushawishi Joan arudi ila juhudi zake zote zimekuwa zikigonga mwamba.

"Anasema kwanza atulie kiasi. Alienda na mtoto. Nilikuwa nataka tuharakishe maisha tufanye mipango mingine" Alisema.

Koech alidaiu alitaka kupata mtoto wa pili mwaka huu juu alikuwa na wasiwasi kwani hapo awali mkewe alikuwa amemtahadharisha ifikapo 2023 hangekubali kupata mtoto mwingine.

Juhudi za kufikia Joan ili apatanishwe na mumewe hata hivyo hazikufua dafu kwani simu yake ilipopigwa ilikuwa mteja.