Patanisho: Mwanadada agura ndoa baada ya mumewe kumpiga vibaya kwa kupika mayai bila ruhusa

Muhtasari

•Brenda alisema watoto wake walishuhudia akipokea kichapo hicho na hata wakajaribu kumzuia baba yao dhidi kuumiza mama yao ila juhudi zao zikaangulia patupu.

•Edwin alifichua kwamba haikuwa mara ya kwanza ya mkewe kuchukua vitu vyake na kuondoka kwani alikuwa ameondoka tena takriban mara saba hapo awali.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Brenda Wamusia (24)  kutoka Webuye alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake  Edwin Wamusia (31).

Brenda alidai ndoa yao ya miaka mitano ilisambaratika mnamo mwezi Agosti wakati aliamua kuondoka na kuacha watoto wao wawili baada ya mumewe kumshambulia vibaya.

Mwanadada huyo alisema aliamua kugura wakati mume wake alimpiga na kumuacha na majeraha mabaya mwilini kufuatia mzozo uliohususisha mayai.

"Alinichapa vibaya nikapata majeraha hadi saa hii figo inaniuma. Kuna kuku nilikuwa nimenunua, ilikuwa inatega mayai na haikuwa na jogoo. Nikamwambia baba Brian kwamba kuku inatega na haina jogoo. Nikachukua mayai kupikia mtoto wangu wa kwanza aende shule. Hiyo kuku ilileta kisirani, jioni kukuja haniongeleshi nikamuuliza kwani hatukuli. Hakunipatia pesa, tukalala hivo. Asubuhi akaamka kama amekasirika akaanza kunichapa. Niliona watoto wangu wamelala njaa nikatafuta namna watakula, hakuwa karibu. Tukakunywa chai kisha akaingia. Nikamuwekea chai akakataa kunywa nikamuuliza mbona hakutaka akaniambia atanimwagia ile chai. Hapo ndipo alianza kunipiga mangumi, akanirusha kwa meza" Brenda alisimulia.

Alisema watoto wake walishuhudia akipokea kichapo hicho na hata wakajaribu kumzuia baba yao dhidi kuumiza mama yao ila juhudi zao zikaangulia patupu.

Brenda alisema aliamua kuondoka mumewe alipokuwa kazini baada ya kutafakari kuhusu kichapo kibaya alichokuwa amepokea. Hata hivyo alidai kwamba angependa kurudi kwani alihofia huenda watoto wake watateseka.

"Saa hii naishi na ndugu yangu Kisii. Niliambia ndugu yangu nahisi siwezi kaa bila watoto wangu nikamsihi aongeleshe mume wangu. Tulifunga safari tukaenda kwangu alafu mume wangu akakataa kuongea na mume wangu" Alisema.

Edwin alipopigiwa simu alisikika mwenye ghadhabu tele  na hata hakutaka kuzungumza na mke wake huku akidai alikuwa amemkosea sana.

Alisema kwamba Brenda alichukua virago vyake akaondoka pekee kwa hiari yake na hakuwa amemfukuza.

Edwin alifichua kwamba haikuwa mara ya kwanza ya mkewe kuchukua vitu vyake na kuondoka kwani alikuwa ameondoka tena takriban mara saba hapo awali.

"Brenda alibeba kila kitu kwa nyumba akasema yeye anaenda kuchukua nyumba aishi pekee yake nikasema kama ameamua ni sawa aende. Si mara ya kwanza, amenisumbua tangu tuoane. Amenisumbua nimefika mwisho kabisa. Ameenda karibu mara saba. Akienda anaenda na vitu zake. Akienda anaenda na hasira na anarudi na hasira. Nilitaka nione wazazi wake huwa ananificha. Sitaki kuongea na yeye" Edwin alisema kwa hasira na akakata simu.

Brenda alisisitiza kuwa mume wake ndiye aliyemfukuza huku akimwambia atoke akafanye ukahaba.

Alisema alishindwa kuvumilia kichapo na matusi ya mume wake. Alidai alikuwa ameondoka nyumbani mara tatu tu.