Patanisho:"Alisema niko na UKIMWI" Mwanadada asimulia jinsi ndoa yake na mwanafunzi wa chuo kikuu ilivunjika kwa kukosa uaminifu

Muhtasari

•Kwa wakati huo alikuwa na ujauzito ila kwa bahati mbaya alipoteza mtoto wake wa kwanza hata kabla hajazaliwa.

•Alisema mume wake ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu aliondoka kwa nyumba alfajiri moja akiwa amebeba vitabu vyake akaenda na hakuwahi rudi tena

Ghost studioni
Ghost studioni

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Atieno (24) kutoka Kisumu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Omondi (22)  walitengana takriban mwezi mmoja uliopita.

Atieno alisema ndoa yao ilivunjika kwa kukosa uaminifu. Kwa wakati huo alikuwa na ujauzito ila kwa bahati mbaya alipoteza mtoto wake wa kwanza hata kabla hajazaliwa.

"Kulikuwa na mambo mengi mazito kwa nyumba. Tulikosana kwa sababu ya mambo madogo madogo na kutoaminiana. Kuna siku nilikuwa nimeenda matanga ya dadangu. Mzee hakuamini nilikuwa nimeenda matanga. Kufika huko akanirushia maneno mengi machafu. Siku nilirudi nikamuuliza jumbe alizokuwa ananitumia zilikuwa za nini. Aliniambia eti nilikuwa nimeenda kufanya ukahaba huko na ndio maana sikuwa nashika simu zake. Tulikuwa na uchungu mwingi kwa wakati ule kwa kuwa hapo awali tulikuwa tumepoteza mjomba alafu tena dada akaaga. Alisema hata niko na UKIMWI. Nilimuuliza makosa yangu hakuelewa. Ana hasira ya haraka na huwa hafuatilii kitu kabla aseme. Ni mtu wa kuropokwa. Saa hii ningekuwa na mtoto na yeye lakini aliaga kabla hajazaliwa"  Atieno alisimulia.

Alisema mume wake ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu aliondoka kwa nyumba alfajiri moja akiwa amebeba vitabu vyake akaenda na hakuwahi rudi tena.

"Bado anasoma. Kuna biashara ndogo ya simu huwa anafanya.. Alitoka saa kumi na moja asubuhi akiwa amebeba vitabu vyake akaenda na hakuniambia mahali anaenda. Kwa kawaida akienda shule alikuwa anatoka kwa nyumba mwendo wa saa mbili, saa tatu hivi. Sina mtoto mwingine" Atieno alisema.

Omondi alipopigiwa simu alipuuzilia mbali madai ya Atieno kuwa hakuwa anamuamini. Alidai kuwa Atieno alikuwa na mazoea ya kukosea mara kwa mara.

Omondi pia alimshutumu mkewe kuwa na mazoea  ya kuzungumza na marafiki wake kuhusu mambo ya mapenzi na ngono, madai ambayo Atieno alikanusha.

"Yeye si mwaminifu, hana heshima. Unajua unafaa kuheshimu mume wako, kila kitu anakwambia unafanya. Yeye alitaka awe juu yangu sielewi. " Omondi alisema.

Jamaa huyo alisema kuna wakati mke wake alikuwa amemkasirikia hadi akakataa kumpikia siku kadhaa.

Atieno alisema huwa anamheshimu mume wake ila akaeleza kuwa wakati mwingine huwa anashindwa kuvumilia kwani mume wake ana mazoea ya kuwa mkali.

"Hawezi kuambia kitu kwa upole,  anakasirika hataki kukuongelesha anakupigia mgongo. Tunaweza kuwa tunakula watu wawili yeye akiwa ameangalia huku hakuongeleshi" Atieno alisema.

Ghost aliwashauri wapenzi hao wawili wawe na mawasiliano mazuri kwa nyumba na wavumiliane kwani wangali wachanga kwa ndoa.