"Anataka mwanamke aende amtafutie kama amelala" Mama mkwe afichua uvivu wa mkwewe

Muhtasari

•Ouma alidai kwamba mke wake alimuacha baada yake kushindwa kumfungulia biashara kama alivyotaka.

•Mama Janetrix alifichua kwamba tatizo kubwa la Ouma ambalo lilimshinikiza binti yake kumtema Ouma ni kuwa yeye ni mvivu.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi jamaa aliyejitambulisha kama Chris Ouma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Janetrix ambaye walitengana takriban miaka miwili iliyopita kufuatia mzozo wa pesa.

Ouma alidai kwamba mke wake alimuacha baada yake kushindwa kumfungulia biashara kama alivyotaka.

Alisema juhudi zake zote za kumrejesha mke wake nyumbani zimekuwa zikigonga mwamba kwani ameendelea kushikilia msimamo wake kwamba hataki kurudi.

"Mwaka jana nilitoka nikaelekea kazini. Mke wangu alikuwa ameniomba nimfungulie biashara lakini kwa wakati huo sikuwa na kazi. Kazi iliyokuwepo ilikuwa ya vibarua lakini haikuwa inaleta kipato kizuri. Nilienda kufanya kazi ya usiku, niliporudi asubuhi nilipata amechukua vitu vyake na kuenda. Nilijaribu kumpigia lakini hatukuwa tunapatana" Ouma alisimulia.

Hatukuweza kumpata Janetrix kwa simu lakini angalau tuliweza kuwasiliana na mama yake.

Mama Janetrix alifichua kwamba tatizo kubwa la Ouma ambalo lilimshinikiza binti yake kumtema Ouma ni kuwa yeye ni mvivu.

"Janetrix anajitetea anasema huyo Chris ni mtu msumbufu. Anasema eti anataka mwanamke aende amtafutie kama yeye amelala. Kila siku akitoka kazini alikuwa anapata huyo jamaa akiwa amelala. Msichana aliona haina maana washinde wakipigana na kuvurugana" Mama Janetrix alisema.

Mama Janetrix pia alifichua kwamba Ouma alimtumia jumbe za matusi baada ya kukosana na binti yake.

Alimshauri mkaza mwana huyo wake abadilishe tabia zake na apange kikao nao ili waweze kusuluhisha mzozo uliopo.

"Mimi niko tayari kusamehe, nakuwanga mhubiri. Mtu akiomba msamaha unamsamehe lakini yule mtaishi naye ndiye unafaa kuomba msamaha. Wewe utazungumza na jamii ya kwenu alafu tukae tuongee. Watu wakiwa na mtoto ukoo huwa haiharibiki, lazima tu itaendelea. Hakuna haja ya matusi kama ile ulituma kwa simu na haujakuja kutuona, tukae tuongee. Tulionelea mtoto wetu hawezi kukaa na mtu kama huyo kwa sababu wewe hauna heshima. Kwa kawaida sisi Waluhya ni watu wenye heshima," Mama Janetrix alisema.

Mama Janetrix alimhakikishia Ouma kwamba mke wake bado yuko nyumbani pamoja na mtoto wao.