Patanisho: Mwanadada azamia katika ulevi baada ya kugundua mumewe ana mpango wa kando

Muhtasari

•Evelyn alikiri kwamba alianza kunywa pombe katika juhudi za kupambana na msongo wa mawazo uliompata baada ya kugundua kuwa mume alikuwa anacheza ngoma nje ya ndoa.

•Alisema angependa waweze kuelewana na mumewe kwanza kabla ya kurudi kwa kuwa ni kawaida yake kugundua umuhimu wa mke wakati tu ako pweke.

Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho mwanadada aliyejitambulisha kama Evelyn alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Daniel Kemboi ambaye walikosana mwezi jana kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Evelyn alisimulia kuwa aligura ndoa yake ya miaka sita baada ya kupigwa vibaya na mumewe wakati alipogundua kuwa alikuwa amejitosa kwenye ulevi.

Alikiri kwamba alianza kunywa pombe katika juhudi za kupambana na msongo wa mawazo uliompata baada ya kugundua kuwa mume alikuwa anacheza ngoma nje ya ndoa.

"Nilipata mume wangu na mambo ya mpango wa kando. Nikijaribu kumueleza hakuwa ananielewa. Ilifika mahali nikawa na msongo wa mawazo nikaona nitumie pombe ili angalay niweze kulala vizuri. Sikujua nilikuwa naharibu maneno. Alipogundua nilikuwa natumia vileo, kuna wakati alinipiga usiku. Asubuhi ilipofika nilitoka nikaenda kwetu" Evelyn alisema.

Evelyn alieleza kwamba ingawa alikuwa amegura ndoa yake, bado kumekuwa na mawasiliano kati yake na mumewe na tayari amefanya juhudi za kumsihi arudi.

Alisema kuwa Kemboi alimhakikishia kwamba tayari amebadilika. Hata hivyo alisema angependa waweze kuelewana na mumewe kwanza kabla ya kurudi kwa kuwa ni kawaida yake kugundua umuhimu wa mke wakati tu ako pweke.

"Nataka tuelewane kwanza. Aliniuliza kama anaweza kutuma nauli nirudi nikamwambia asubiri jibu... Naumia sana na watoto. Nilipata ushauri kuhusu msongo wa mawazo. Hiyo ilinitoka, sasa niko sawa" Evelyn alisema

Juhudi za kuwapatanisha wawili hao hata hivyo ziligonga mwamba kwa kuwa Kemboi hakupatikana kwa simu.