Patanisho: Jamaa ashtumiwa kwa uchawi baada ya wanawe wawili kuaga, mkewe kutopata mimba tena

Leah alisema hajaweza kupata mimba tena baada ya watoto wake wawili kufariki nyakati tofauti.

Muhtasari

•Leah alifichua kuwa watoto wawili ambao alipata na Saul waliaga dunia, tatizo ambalo hajui limesababishwa na nini.

•Saul alisema mke huyo wake wa zamani aliondoka nyumbani mwenyewe bila kushinikizwa wakati yeye akiwa kazini.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Leah Nawire ,26, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Saul ,40, ambaye alikosana naye mwezi Novemba mwaka jana.

Leah alisema ndoa yake ya miaka sita ilisambaratika baada ya mienendo ya mumewe kwa nyumba kuanza kubadilika.

Aidha, alifichua kuwa watoto wawili ambao alipata na Saul waliaga dunia, tatizo ambalo hajui limesababishwa na nini.

"Ndoa yangu ni ya miaka 6. Tulikuwa tunakaa vizuri alafu tukapata watoto wawili na yeye. Nilimpata na watoto wawili wasichana.Mimi sijaweza kulea watoto wangu. Wa kwanza aliaga, alafu wa pili akaaga pia," alisema.

Leah aliweka wazi kwamba hajaweza kupata mimba nyingine baada ya kupoteza watoto wake wawili wa kwanza.

"Miaka nne imeisha sasa, sijapata mimba ingine tena. Sijui shida ni nini. Maneno mengine mengi pia yametokea," alisema.

Aliongeza,"Tayari tumeenda kwa daktari. Daktari alisema kwamba mimi niko sawa, niliambiwa labda yeye ashughulikiwe. Sasa hashiki simu yangu. Nilitoka huko mwezi Novemba. Sasa hivi niko Ruiru."

Bw Saul alipopigiwa simu alisema alipitia masaibu mengi wakati wa mahusiano yake na mke huyo wake wa zamani.

"Huyo mrembo niliona mambo yake ni ngumu. Aliingiza watu wa kwao. Kuna fitina nyingi alileta mimi nikaona ni ngumu," alisema.

Saul alisema mke huyo wake wa zamani aliondoka nyumbani mwenyewe bila kushinikizwa wakati yeye akiwa kazini.

"Nilipata  kamamlango imefungwa na amebeba kila kitu akaenda. Nyanyake alisema nafaa niende huko tu tuongee lakini akasema kwamba msichana wake ameteseka sana tukiwa na yeye," alisema.

Saul alisema kwamba familia ya mkewe ilimnyooshea kidole cha lawama na kumshtumu kwa uchawi baada ya watoto wao wawili kuaga, jambo ambalo lilimshangaza sana na kumsikitisha. 

"Nilimpata nikiwa na watoto wawili wasichana. Alipata mimba na mtoto wa kwanza akatoka. Mara ya pili akazaa vizuri lakini akaaga pia. Watu wa kwao walianza kusema sisi ni wachawi, nilishangaa sababu mimi tayari niko na watoto wawili. Nyanya yake aliniambia nikasikia vibaya sana," alisema.

Alidai kwamba baada ya Leah kutoroka alijaribu kufuatilia ili kumrejesha ila juhudi zake hazikufua dafu.

"Kwa upande huu nishamove on. Tayari niko na mke mwingine. Tumekaa mwezi moja sasa," alisema.

Leah hakuwa na budi ila kukubali uamuzi wa mume huyo wake wa zamani na kukubali kusonga mbele na maisha yake.

"Ni sawa basi kama ameamua," alisema.