Patanisho: Jamaa atangaza anatafuta mke kwenye Facebook licha ya kuwa katika ndoa tayari

Evans alikiri kuwa ndoa yake ya miaka miwili ilivurugika baada ya mkewe kumpata na mpango wa kando.

Muhtasari

•Evans alikiri kuwa ndoa yake ya miaka miwili ilivurugika mwezi uliopita baada ya mkewe kumpata na mpango wa kando.

•Janel alifichua kuwa mumewe alikuwa ametangaza kwamba anatafuta mke kupitia Facebook licha ya kuwa na mke na mtoto

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi, Evans Onyancha (27) kutoka Nyamira alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Janel Muleshi (25).

Evans alikiri kuwa ndoa yake ya miaka miwili ilivurugika mwezi uliopita baada ya mkewe kumpata na mpango wa kando.

"Tulikuwa marafiki na mwanadada huyo. Nilikuwa naambia mke wangu naenda safari. Alikuwa amesikia nikongea na mpango huyo wa kando kwa simu, nilimwambia mke wangu kuwa huyo ni mteja," Evans alisimulia.

Aliongeza,"Alinipata na mpango wa kando Nyamira. Tulikuwa tumeachana naye kitambo na nikamwambia kuwa tayari nimeoana, sijui mbona alinifuata," 

Evans alikiri kuwa anajuta sana kumkosea mkewe na kuomba asaidiwe kumshawishi arudi nyumbani.

Janel alipofikiwa kwa njia ya simu alimhoji mumewe kuhusu sababu zake kutoka nje ya ndoa. Alimshtumu baba huyo wa mtoto wake mmoja kwa kuharibu ndoa yao.

"Mimi nilikufinya kwa nyumba ndio ukaenda kutafuta mwingine huko nje? Wee ndo uliharibu ndoa yako. Hiyo miaka yote tulikaa na wewe sijawahi kukunyima mapenzi ili uende kutafuta nje" Janel ambaye alisikika mwenye ghadhabu kubwa alimuuliza mumewe.

Alifichua kwamba Evans amekuwa akikosea mara kwa mara na kurudia kosa hata baada ya kusamehewa.

Pia alifichua kuwa mumewe alikuwa ametangaza kwamba anatafuta mke kupitia Facebook licha ya kuwa na mke na mtoto.

"Sio mara yake ya kwanza kukosea. Huwa namsamehea alafu anarudia tena.. Uko na bibi alafu unapost kwa Facebook eti unatafuta bibi!" Alisema.

Janel hata hivyo alikiri kuwa hana kinyongo dhidi ya mumewe na kusema kuwa yupo tayari kurudiana naye. Hata hivyo alimpatia Evans sharti kuwa lazima apige hatua ya kuzungumza na wazazi wake kabla yao kurudiana.

"Apige simu nyumbani aongee na wazazi. Mimi sina chuki naye. Mimi nilimsamehe hata kabla akuje Radio Jambo,"

"Hiyo tabia yako ya kuhanyahanya utakoma. Maisha ya saa hii sio ya kuzurura kuna magonjwa. Mimi bado nakupenda," Janel alimwambia mumewe.

Evans aliahidi kubadili tabia zake huku akimshukuru mumewe kwa kukubali ombi lake la msamaha.

"Nakupenda kama nyama choma. Sitaki nirudie kosa hilo tena. Hilo nakuhakikishia," Alisema.

Baada ya Patanisho hiyo kuzaa matunda Gidi aliwatakia wapenzi hao kheri njema na furaha katika ndoa yao.