Vitambulisho Elfu Tano Bado Kuchukuliwa Migori

Huku wakenya wakijitayarisha kwa kampeni za kisiasa na uchaguzi mkuu wa Agosti mwaka huu zaidi ya vitambulisho elfu tano bado havijachukuliwa na wenyewe katika afisi za msajli wa watu kwenye kaunti ya Migori.

Kulingana na mkurugenzi wa usajili wa watu kwenye kaunti ya Migori Seth Mboya, vitambulisho hivyo elfu tano kutoka gatuzi nane za kaunti hiyo vimesalia katika afisi hiyo tangu mwishoni mwa mwaka uliopita na kutaka wenyewe kuja kuvichukua.

Mboya alikuwa akihutubia wanahabari afisini mwake wakati wa uzinduzi wa shughuli za kupiga msasa na kufanyia uchunguzi mwafaka wale wanaotaka kujisajili kuchukua vitambulisho katika kaunti hiyo.

Aliwataka machifu na manaibu wao wanaohudumu katika maeneo ya mpakani mwa Kenya na Tanzania kuwa waangalifu zaidi wanapofanya ukaguzi na kupiga msasa vijana wanaotaka vitambulisho ndiposa wasiweze kusajili raia kutoka nchi jirani ya Tanzania.