Katika arifa ya gazeti rasmi la serikali iliyochapishwa Juni tarehe 23 maseneta wametakiwa kuwa katika bunge la senate saa nane unusu mchana siku ya Ijumaa.
Gavana huyo ameshtumiwa na wawakilishi wa kaunti waliomuondoa afisini kwa kutumia vibaya afisi yake, kukiuka katiba na kukiuka sheria za uagizaji wa bidhaa.
Pia anashtumiwa kwa kujitengea shilingi milioni 10 kama marupurupu yake ya usafiri.
Waiguru ameyataja madai hayo kama wongo na njama ya kuhujumu uongozi wake. Akijitetea mbele ya kamati ya wanachama 11 siku ya Jumatano, Waiguru amesema anapigwa vita kwa sababu ya kuunga mkono mchakato wa BBI.
Endapo kamati hiyo itapata uhalali wa mojawapo ya madai yanayotolewa na wawakilishi hao huenda wakaidhinisha uamuzi wao wa kumfurusha Waiguru afisini. Uamuzi huo hata hivyo utafanywa kupitia kura ya maseneta.
Endapo madai hayo yatapuuzwa na wanachama wengi basi hoja hiyo itashindwa.