Waititu atapatapa akitaka Uhuru amsaidiye katika kesi ya ufisadi dhidi yake

Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi amejaribu kila mbinu akitaka kesi dhili yake kusitishwa.

Mbali na kutaka usaidizi kutoka kwa Naibu rais William Ruto, gavana huyo pia amekuwa akijaribu kumtafuta rais Uhuru Kenyatta amsaidiye. Rais Kenyatta bado hajakutana na Waititu lakini gavana huyo amekuwa akihudhuria hafla za rais akiwa na matumaini ya kuzungumza naye.

Gavana Waititu pia amemuandikia barua mkurugenzi wa mashtaka ya umma Noordin Haji akiomba pawepo maafikiano baina yao ili kesi yake isitishwe, lakini ombi hilo pia liliambulia patupu.

Waititu na mkewe Susan Wangari walifikishwa mahakamani mwezi Julai wakikabiliwa na mashtaka sita kuhusiana na dosari katika taratibu za utoaji wa zabuni ya kima cha shilingi milioni 580. Jana Waititu hakukubali au kukataa juhudi zake kujaribu kusitisha kesi dhidi yake.

“Nani alikwambia,” Alifoka.

Wakati wa mazishi ya mamake Peter Kenneth, Rahab Wambui mwezi Julai, Waititu alijaribu sana kuzungumza na rais kuhusu kesi yake.

“Alipopata nafasi alimuomba rais kumsaidia ili kesi yake itupiliwe mbali lakini rais alimuambia aubebe msalaba wake mwenyewe .,” Jamaa wa karibu na wawili hao alisema.

Siku ya Jumatano Waititu alijaribu tena bila mafanikio kuzungumza na rais Kenyatta katika hafla ya uzinduzi wa huduma za gari moshi kati ya Nairobi na Naivasha.

Walinzi wa rais walihakikisha hamkaribii rais hata alipotaka kujiunga na magavana Alfred Mutua wa Machakos, Joseph Ole Lenku wa Kajiado na Mike Sonko wa Nairobi katika hafla ya upigaji picha na Rais Uhuru Kenyatta.

“Nilikuwepo kama gavana wa Kiambu. Nini kilikuwa kibaya na kuwepo kwangu?” Waititu aliuliza.