Waluke apewa dhamana ya Shilingi milioni 10 ,Wakhungu milioni 20

Waluke
Waluke
Mbunge wa Sirisia John waluke  ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 10 pesa taslimu  ilhali mtuhumiwa mwenzake Grace  Wkhungu ameachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 20 katika kesi ya ulaghai unaohusisha shilingi milioni 313 za shirika la NCPB.

Jaji John Onyiego  jumatatu ameagiza kwamba  wawili hao wazisalimishe paspoti zao kortini  .Hawataruhsiwa kusafiri nje ya nchi hadi  rufaa yao iamuliwe .

Onyiego  amesema ameshawishika kwamba wawili hao wana msingi wa kuwasilisha rufaa . Waluke na Wakhungu walishtakiwa kwa njama ya kuilaghai NCPB shilingi milioni 313 .

Wakhungu  alikuwa awali amehukumiwa kifungo cha miaka 69 jela akiwa na chaguo la kulipa faini ya shilingi bilioni moja ilhali Waluke alikuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 67 gerezani na chaguo la kulipa kiasi hicho cha faini .

Kuhusu Waluke kudai kwamba huenda akapoteza kiti chake cha ubunge ,jaji Onyiego amesema sheria ni sawa kwa kila mtu na hakuna atakayepewa   adhabu tofauti kwa msingi wa hadhi au wadhifa wake.