Wanafunzi kupewa mafunzo dhidi ya ugaidi

Hayatakuwa mafunzo tu ya Hesabu, Kiswahili na Sayansi pekee. Shule zitalazimika kuwapa wanafunzi mafunzo dhidi ya ugaidi, mbinu za kutambua vilipuzi na hatua za kuchukuwa wakati kuna shambulizi, ikiwa mswada unaopendekezwa utapitishwa bungeni.

Mswada huo uliowasilishwa na mwakilishi wa kina mama wa Turkana Joyce Emanikor unalenga kupunguza athari zinazotokana na mabomu haswa vilipuzi vinavyotegwa ardhini (IED). Haya ni mabomu yaliotengenezwa nyumbani na kutegwa katika njia zisizo za kawaida, sanasana kwenye mabarabara.

Kundi la kigaidi la Al Shabaab limekuwa likilenga vikosi vya usalama wa Kenya, majumba ya kibiashara, mahoteli na taasisi za masomo kwa kutumia vilipuzi vya kujitengenezea na silaha zinginezo. Emanikor atarajia kuwa mswada wake utawapa wanafunzi msingi unaohitajika ili kufikiria haraka na kujiandaa kukabiliana na hali ya hatari wakati wa uvamisi kama ilivyokuwa katika shambulizi la kigaidi katika chuo Kikuu cha Garissa.

Ikiwa mswada huo utaidhinishwa kuwa sheria, mtaala wa masomo utapanuliwa kujumuisha mafunzo ya miigo ya kujiepusha na uvamizi, huduma ya kwanza, mbinu za kutambua vilipuzi, kutambua hatari miongoni mwa mafunzo mengine ya kiusalama.

Mswada huu “Kenya Institute of Curriculum Development (Amendment ) Bill, 2019.” Hata hivyo hauelezi ni katika kiwango kipi cha elimu mwanafunzi anapaswa kupoka mafunzo haya.

Kwa sasa mswada huo unajadiliwa na kamati ya bunge ya elimu kabla ya kurejeshwa bungeni kwa awamu ya pili ya kusomwa kwake.