Wasichana walioacha masomo kutokana na mimba za mapema waregeshwe shuleni - Margaret Kenyatta

Margaret kenyatta
Margaret kenyatta
Mama wa Taifa Margaret Kenyatta anataka wasichana walioacha masomo baada ya kutunga mimba na kuzaa kuregeshwa shuleni ili kuwapa fursa ya kukamilisha masomo yao.

Alisema mimba za mapema hazifai kuwa mwisho wa masomo ya wasichana hao au kuwatupa mama hao wachanga katika dhiki na umaskini unaotokana na kukosa masomo.

Mama wa Taifa wa Kenya alisema hayo katika Kituo cha Wanawake cha Wakfu wa Wanawake jijini Kingston Jumatatu ambapo alikuwa mgeni wa heshima.

Alizungumza na kundi la mama wachanga ambao wamefaulu kuregeshwa shuleni kupitia kwa mpango maalum wa mama wachanga.

Mama wa Taifa anaandamana na Rais Uhuru Kenyatta ambaye anafanya ziara ya kiserikali ya siku tatu katika mataifa ya Carribean.

“Nimeunga mkono miradi kwa dhati – kama huu ambao unahimiza wasichana kubaki shuleni ili kunufaika na elimu bila kujali hali zao. Ninaamini kwa kweli katika ahadi ya tumaini ambayo elimu huwapa na kuwawezesha wasichana wetu,” kasema Mama wa Taifa Margaret Kenyatta.

Alisema kudumisha wasichana shuleni hupunguza moja kwa moja kiwango cha visa vya vifo vya akinamama wazazi na hulinda wanawake wachanga kutokana na maambukizi ya Ukimwi.

Akitumia mfano wa Kenya, Mama wa Taifa alisema wasichana huzuiwa kuafikia elimu kikamilifu na changamoto nyingi zikiwepo umbali wa shule na nyumbani mwao na shida za kifedha zinazokumba familia nyingi na kusababisha wasichana kubaki nyumbani kushughulikia ndugu zao.

Desturi hatari kama vile ndoa za mapema na upashaji tohara kwa wanawake ni mojawapo ya vizuizi vingine vinavyotatiza elimu ya wasichana ambavyo vilitambuliwa na Mama wa Taifa.

“Tunafanya bidii kutafuta suluhisho za shida hii kama mpango huu ili kuhakikisha wasichana hawawachi masomo. Tunahimiza jamii kuwaregesha wasichana wazazi shuleni,” kasema Mama wa Taifa akiongeza kwamba Kenya inahitaji kujifunza kutokana na mfumo wa elimu wa Jamaica.

Mkewe Rais ambaye mwenyeji wake katika kituo hicho alikuwa Mama Allen Patrick, Mkewe Gavana Mkuu wa Jamaica akiandamana na Waziri wa Michezo Olivia Grange alisema kuna mamilioni ya wasichana waliohatarini kote duniani ambao wanahitaji msaada ili kuafikia ndoto zao katika elimu lakini ni vigumu kupata nafasi na msaada wanaohitaji kuwawezesha kufanikisha ndoto hizo.

“Sote tunataka wasichana kupata maisha mema ya usoni, lakini hatuwezi kusahau kwamba bado kuna wasichana wanaohitaji fursa hizo lakini hawawezi kuzipata,” kasema Mama wa Taifa.

Alipongeza mwenyeji wake kwa mpango huo wa ubunifu mkubwa na akapongeza wanafunzi wa sasa kwa uvumilivu wao dhabiti na kwa kutambua umuhimu wa elimu kama kifunguo cha maisha ya usoni.

Bali na kutoa elimu kwa akina mama wachanga, kituo hicho hutoa huduma za ushauri nasaha wa afya, familia na maisha, ulezi na utoaji wa huduma za rufaa kwa wanawake na wanaume.

Tangu kuanzishwa kwa kituo hicho miaka 40 iliyopita, zaidi ya mama wachanga 46,000 wamepitia katika mpango huu, baadhi yao wakiweza kuwa watu mashuhuri katika jamii ya Jamaica.

“Nahimiza nyinyi nyote wasichana kutumia vyema zaidi fursa hii kukuza talanta zenu na kuafikia upeo wa juu zaidi,” Mama wa Taifa aliwaambia wasichana hao.

Aliwahimiza wasichana hao wazazi kutia bidii kufaulu katika masomo yao na kukuza wasifa na kuafikia ndoto zao za kuwa wanawake waliofaulu.

-PSCU