Wololo! Gavana Mandago awafurusha wanafunzi 700

Gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago amewafurusha wanafunzi mia saba walioeka mkataba na serikali ya kaunti hiyo kwa madai kuwa walikataa kuondoka baada ya muda wa mkataba wao kukamilika.

Gavana huyo amesema kuwa serikali yake iliandikisha mkataba wa mwaka moja na wanafunzi hao waliohitimu kutoka vyuo vikuu ambao ulikamilika miezi mitatu iliyopita huku akiwataka wanafunzi hao waondoke ili wawapishe wenzao wapate ile uzoefu wa kazi huku akiongezea kuwa mkataba huo haukutaja mahali popote kuwa serikali yake itawaajiri wanafunzi hao.

Wanafunzi hao ambao walihudumu katika idara mbalimbali katika kaunti hiyo, walikuwa wanapata malipo kati ya elfu kumi na elfu kumi na tano kwa muda wa miezi kumi na mbili.

Hayo yakijiri, baadhi ya viongozi wa zamani katika kaunti ya Taita Taveta wamemtaka gavana Granton Samboja kukubali kufanya mazungumzo na wawakilishi wadi ili kusitisha mzozo wa bajeti unaoendelea.

Wakiongozwa na aliyekuwa gavana John Mruttu na aliyekuwa seneta Dan Mwazo, wamesema kuna haja ya Samboja kuwapa nafasi viongozi wa kidini ili kupatanisha pande zote mbili.