Yaya Ahukumiwa Maisha Kwa Kumdunga Mwenziwe Kisu

Yaya mmoja wa umri wa miaka 42 amehukumiwa maisha kwa kumdunga kisu mwenzake miaka miwili iliyopita walipozozania kikombe cha chai.

Mahakama ya Kibera imempata Dinah Mbaah na hatia ya kutekeleza kosa hilo. Polisi wanasema Mbaah alimdunga Josephine Mutuku kisu cha shavuni katika mtaa wa Kileleshwa jijini Nairobi mwaka 2015. Hakimu Jane Kamau anasema upande mashtaka ulitoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha kosa hilo.

Mwathiriwa ameiambia mahakama kwamba alikua jikoni wakati yaya huyo alipofika akitaka kupewa chai  Jane anasema alimuonya mshukiwa kutojiwekea chai lakini akakasirika na kumtusi.

Mshukiwa ambaye ni mama wa watoto watatu baadaye alimsukuma na kumwangusha chini kisha akachukua kisu na kumdunga shavuni, kisu kilichopenya hadi upande mwingine wa shavu.

Baada ya kutekeleza kosa hilo mshukiwa Mbaah aliruka ukuta akijaribu kutoroka lakini polisi waliokua wamearifiwa na mlinda lango walimkamata.

Daktari aliyetoa ushahidi katika kesi hiyo anasema Mutuku alijeruhiwa vibaya na kwamba walipendekeza afanyiwe upasuaji ikizingatiwa kwamba alipoteza meno kadhaa na hivyo akawa hawezi kutafuna chochote.

Lakini mshukiwa anasema hakudhanmiria kumshambulia Mutuku. Ameomba kusamehewa kwa sababu yeye ni mjane.

Ana wiki mbili kukata rufaa katika mahakama kuu.