Jamaa wanne wa familia waliouwawa Karura kuzikwa leo

Familia ya Warunge
Familia ya Warunge

Watu wanne wa familia moja waliouwawa kikatili nyumbani kwao katika eneo la Karura kaunti ya Kiambu watazikwa hii leo.

Wanne hao pamoja na mfanyikazi wa shambani wanadaiwa kuuwawa na jamaa yao Lawrence Warunge ambaye sasa atakabiliwa na mashtaka ya mauaji baada ya uchunguzi wa akili kuthibitisha kuwa ana uwezo wa kuhukumiwa.

Uchunguzi wa maiti uliofanywa Jumanne ulifichua kuwa watano hao waliuwawa kutokana na majeraha kadhaa ya kudungwa kisu ambayo huenda yote yalisababishwa na mtu mmoja tu.

Ifuatayo ni mkusanyiko wa habari mbalimbali humu nchini;

Polisi wamemkamata mwanaume mmoja katika eneo la Ruiru kaunti ya Kiambu kwa madai ya kutuma jumbe mbili fupi za kumtishia maisha seneta wa Murangá Irungu Kang'áta.

Kukamatwa huko kunafuatia lalamiko lililowasilishwa na Kang'ata Januari tarehe 7 kwenye makao makuu ya DCI.

Mshukiwa huyo Michael Chege anadaiwa kumtishia Kangata kuhusu maoni yake ya  ufahamu wa BBI katika eneo la Mlima Kenya kama alivyoandika kwenye barua yake kwa Rais.

Huku wiki ya pili tangu shule kufunguliwa ikikamilika jana , serikali inasema asilimia 96 ya wanafunzi wa shule za sekondari wamerejea shuleni nazo shule za msingi zimesajili asilimia 95 ya wanafunzi. Waziri wa elimu George Magoha anasema baadhi ya wanafunzi ambao wangali kurejea wako katika maeneo yanayohitajika kuwa na chakula ili warejee shuleni.

Asasi za kiraia  humu nchini yanadai  kuwachiliwa kwa wafuatiliaji wa uchaguzi 26 wanaodaiwa kukamatwa  siku ya Alhamisi na maafisa wa polisi wa Uganda  na kuzuiliwa katika vituo tofauti vya polisi. Makundi hayo yanasema 26 hao walikamatwa kufuatia malalamishi ya kamati ya uchaguzi ya nchi hiyo kwamba kituo chao kilikuwa kinatumika kuhesabu kura kinyume cha sheria.