"Natumai kuolewa, ila sio lazima" Mwanasoshalaiti Amber Ray azungumzia suala la mahusiano

Muhtasari

•Takriban miezi miwili baada ya kutengana na aliyekuwa mpenzi wake mfanyibiashara Jimal Rohosafi, Ray ameweka wazi kwamba kwa sasa hana mchumba na kusisitiza kuwa hayuko katika harakati za kutafuta mwenza.

•Ray amesisitiza kwamba hana mipango ya kuacha kuponda raha hivi karibuni na atapumzika tu wakati ataaga dunia na kuzikwa,

Image: INSTAGRAM// AMBER RAY

Mwanasoshalaiti mashuhuri nchini Faith Makau almaarufu kama Amber Ray amesema kwamba ana matumaini ya kufunga ndoa siku moja.

Alipokuwa anashirikisha mashabiki katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, mama huyo wa mtoto mmoja hata hivyo alisema kwamba hatua ya kufunga ndo sio ya lazima maishani mwake.

"Natumai kuolewa, lakini sio lazima" Amber Ray alisema. 

Takriban miezi miwili baada ya kutengana na aliyekuwa mpenzi wake mfanyibiashara Jimal Rohosafi, Ray ameweka wazi kwamba kwa sasa hana mchumba na kusisitiza kuwa hayuko katika harakati za kutafuta mwenza.

"Niko single na wala sitafuti" Alisema Ray.

Hata hivyo ameeleza kwamba hakuna ugomvi wowote kati yake na mfanyibiashara huyo mashuhuri aliyekuwa amemuoa kama mke wa pili.

Amber Ray alipoulizwa kwa sasa anachumbia nani alidai kwamba anajichumbia mwenyewe.

Ray pia alipuuzilia mbali uvumi uliodai kwamba wako kwenye uhusiano wa mapenzi na mchekeshaji Eric Omondi.

Hivi karibuni uvumi kuwa wawili hao huenda wameamua kujitosa kwenye mahusiano ulienezwa mitandaoni baada yao kuwasiliana hewani kwenye mtandao wa Instagram huku wakiitana majina matamu ya mapenzi.

Hata hivyo, Amber Ray amesema kwamba uhusiano wake na Eric ni wa kibiashara tu..

"Hatuchumbiani,, hiyo ni biashara tu" Amber Ray alisema.

Mwanasoshalaiti huyo amedai kwamba kwa sasa haangazi suala la mahusiano ila anataka tu kuchapa kazi na kujipatia utajiri  mkubwa.

Hata hivyo, Ray amesisitiza kwamba hana mipango ya kuacha kuponda raha hivi karibuni na atapumzika tu wakati ataaga dunia na kuzikwa,

Ndoa kati ya Amber  Ray na Jimal ambayo ilikuwa imejawa na sarakasi si haba iligonga mwamba ghafla mnamo mwezi Julai baada ya wawili hao kuchumbiana kwa kipindi kifupi kifupi.