"Nilikuwa nalia sana!" Nana Owiti afunguka kuhusu masaibu aliyopitia wakati King Kaka alikuwa amelazwa hospitalini

Muhtasari

•Nana  alifichua alikuwa anajiandaa kuanza shoo wakati alipigiwa simu kuambiwa mume wake alikuwa amezidiwa na ugonjwa.

•Nana alisema licha ya kuwa hali ya afya ya mumewe ilikuwa inazorota alikuwa anahofia kumwambia akalazwe kwani yeye mwenyewe akubali kupelekwa hospitalini wakati atataka. 

•Nana alisema kwa wakati mwingine alikuwa analala katika chumba cha hospitali ambacho King Kaka alikuwa amelazwa.

Nana Owiti na King Kaka
Nana Owiti na King Kaka
Image: INSTAGRAM// KING KAKA

 Nana Owiti amefunguka kuhusu masaibu ambayo alipitia wakati mume wake, King Kaka alikuwa amelazwa hospitalini.

Akiwa kwenye mazungumzo na mwamuziki huyo hivi majuzi Nana ambaye ni mtangazaji katika kituo cha Switch TV alifichua alikuwa anajiandaa kuanza shoo wakati alipigiwa simu kuambiwa mume wake alikuwa amezidiwa na ugonjwa.

Wakati huo sio King Kaka pekee aliyekuwa mgonjwa ila aliarifiwa kwamba pia mwanawe alikuwa anaugua.

Habari hizo zilivunja moyo wa mtangazaji machozi yakaanza kumtiririka h hadi akashindwa kuendeleza shoo yake.

"Nilikuwa kazini. Vile tuliingia tu baada ya kufanya mic test na tuko karibu kuenda hewani, takriban dakika 10-15 kabla ya kuenda hewani kijakazi wetu Christine akanipigia simu akaniambia eti mtoto wetu ni mgonjwa na anatapika, ako na homa. Mimi niliisha nguvu, Kaka ni mgonjwa alafu pia mtoto wangu ni mgonjwa. King Kaka akazidiwa. Nikapigia jirani kuuliza kama ako nyumbani lakini hakuwa... Chairman ndiye alikukujia (King Kaka)  akakupeleka hospitali. 

Singeweza kufanya shoo. Machozi ilikuwa inanitoka, producer wangu alikuja haraka kwa studio akaniuliza tatizo ni nini. Tayari nilikuwa nimetaja huskii vizuri kwa sababu wakati mwingine nilikuwa nachelewa kazini" Nana alisema.

Kwa kuwa hangeweza kuendeleza shoo, Nana aliachia mtangazaji mwenzake jukumu hiyo na akaanza safari ya kuenda hospitali kuona mumewe alivyokuwa anaendelea.

Nana alisema licha ya kuwa hali ya afya ya mumewe ilikuwa inazorota alikuwa anahofia kumwambia akalazwe kwani yeye mwenyewe akubali kupelekwa hospitalini wakati atataka. 

"Sikutaka iwe mimi nitasema unahitaji kulazwa kwa sababu hukuwahi kuwa mgonjwa hapo awali. Nilitaka sana itoke kwako. Uliposema utalazwa nilianza kufunga mifuko"  Nana aliambia King Kaka.

Nana alisema kwa wakati mwingine alikuwa analala katika chumba cha hospitali ambacho King Kaka alikuwa amelazwa.

Alikiri kwamba angebaki kazini kwanza akilia ili atakapofika hospitali aweze kupatia mumewe nguvu ya kupigana na ugonjwa na asimuonyeshe machozi.

"Nilijua siwezi kuonyesha (King Kaka) udhaifu, lazima ningekuwa nguvu yako. Hiyo ilimaanisha singelia nikuonyeshe eti napoteza matumaini... Nilikuwa nalia sana haswa baada ya shoo. Lakini wakati nafika kwa hospitali ningekuwa nishamaliza na hata nikajipanguza vipondozi niko tu sawa. Lakini ilikuwa inashtua sana" Nana alisema.

Alieleza sababu za kuenda kazini licha ya kuwa mumewe alikuwa anaugua ni ili aweze kupata utulivu kufuatia masaibu aliyokuwa anapitia nyumbani na ili asiachie wafanyikazi wenzake mzigo mkubwa kazini.