Kate Actress asimulia wazazi wake walivyosikitika alipopachikwa ujauzito miezi 3 baada ya kujiunga na chuo kikuu Uganda

Muhtasari

•Cate alisema alitumia fursa aliyopata katika chuo kikuu kuponda raha kuanzia siku za kwanza kwanza na alishtuka sana wakati daktari alipomvunjia habari kuhusu ujauzito wake.

•Mwigizaji huyo alifichua kuwa mama yake alikuwa amechukua mkopo wa laki nne ili kumpeleka katika chuo kikuu Uganda.

•Cate alisema jamaa ambaye alikuwa amempachika ujauzito alimsaidia siku za kwanza lakini baada ya kuona mambo yanaendelea kuwa mazito akamuacha.

Catherine Kamau
Catherine Kamau
Image: INSTAGRAM

Mwigizaji mashuhuri Catherine Kamau almaarufu kama Cate Actress amefichua alibeba ujauzito wa kifungua mimba wake miezi mitatu tu baada ya kujiunga na chuo kikuu cha Kampala nchini Uganda.

Alipokuwa kwenye mahojiano na Daniel 'Churchill' Ndambuki katika kipindi cha Churchill show, mwigizaji huyo alisema alishangazwa sana na  uhuru ambao alipata alipojiunga na chuo kikuu  kuona kuwa mama yake alikuwa amemkazia raha kabla ya kuelekea Uganda.

Cate alisema alitumia fursa aliyopata katika chuo kikuu kuponda raha kuanzia siku za kwanza kwanza na alishtuka sana wakati daktari alipomvunjia habari kuhusu ujauzito wake.

"Ilikuwa kama uhuru. Ningeweza kuenda nje. Tulikuwa  karibu na Kabaragala, hepi kila wakati.. tulidunda. Hata sikupumua, miezi mitatu nikabeba ujauzito. Sikuelewa jinsi ilikuwa mshtuko kwangu, ilikuja haraka. Hata daktari aliponiambia sikuamini. Nilikuwa msichana mdogo na mtu hangejua. Sikufahamu kuhusu kutumia mbinu za kuzuia ujauzito. Niliendea dawa za 'Morning after' baada ya wiki tatu " Cate alisimulia.

Mwigizaji huyo alifichua kuwa mama yake alikuwa amechukua mkopo wa laki nne ili kumpeleka katika chuo kikuu Uganda.

Wakati aliporudi nyumbani baada ya kujua kuhusu ujauzito wake, mama yake alikuwa amesafiri nje ya nchi. Cate aliacha kama ameandikia mamake barua kisha kuenda kwa rafiki yake akisubiri kujua jinsi angechukulia habari hizo.

"Mama yangu alikuwa amesafiri kuenda nje ya nchi niliporejea. Tulikuwa na babangu kwa nyumba na hakujua. Siku moja kabla ya mamangu kurejea nilimwandikia barua refu kisha nikatoweka kuenda kwa rafiki yangu kwa kipindi cha wiki moja. Mama alipokuja alisoma barua akapigwa na butwaa. Alijua mahali nilikuwa, baada ya wiki moja akaambia rafiki yangu aniambie nirudi nyumbani" Alisema.

Alisema hali haikuwa nzuri pale nyumbani aliporejea kwani wazazi wake walisikitishwa sana na habari zile. 

"Siwezi taka kuona wazazi wangu wakiwa wamesikitika hivo tena. Ilikuwa mbaya, kama kifungua mimba ilikuwa jambo mbaya" Alisema.

Cate alisema jamaa ambaye alikuwa amempachika ujauzito alimsaidia siku za kwanza lakini baada ya kuona mambo yanaendelea kuwa mazito akamuacha.

Alieleza mama yake alimfunza jinsi ya  kuwa mama mzuri kwa kipindi cha miaka miwili kabla  ya kumrudisha shule.

"Nilipata mtoto nikatulia. Mama yangu alihakikisha nimejua jinsi ya kuwa mama. Nilikaa miaka miwili nyumbani, nilikuwa msaidizi nyumbani, nilikuwa nafanya kila kitu kwa takriban miaka miwili. Nilikuwa nafua nepi. Marafiki na binamu zangu walikuwa wanenda nje ilhali mimi sikuwa na uhuru huo. Nilijifunza, nilihisi uchungu huo. Ilikuwa jambo nzuri lakini" Cate alisema.

Baada ya kuwajibikia mtoto wake kwa miaka miwili mwigizaji huyo alipelekwa katika shule kikuu cha Multimedia kupata masomo ya uandishi wa habari ila hakumaliza.