"Hatukuwa tunapendana!" Cate Actress afunguka kuhusu ndoa yake na Philip Karanja

Muhtasari

•Cate alifichua walipokuwa wanajuana uhusiano wao  haukuwa mzuri  vile kwani Karanja hakuwa anapendezwa na mienendo yake.

•Alisema kwa wakati ule Karanja hangewahi amini kuwa siku moja wangekuwa mume na mke.

•Alifichua kuwa yeye ndiye alimshinikiza mumewe wafunge ndoa kwa kuhofia asije akaachwa siku moja.

Philip Karanja na Catherine Kamau wakati wa harusi yao
Philip Karanja na Catherine Kamau wakati wa harusi yao
Image: HISANI

Mwigizaji Catherine Kamau almaarufu kama Cate Actress amefichua hakuwahi fikiria atawahi funga ndoa na mpenzi wake mwigizaji Philip Karanja.

Alipokuwa kwenye mahijiano na Daniel 'Churchill' Ndambuki katika kipindi cha Churchill show, mama huyo wa watoto wawili alisema walijuana na mumewe katika kipindi cha Mother in-law ambapo alikuwa anaigiza kama 'Celina' ilhali Karanja alikuwa mwelekezaji filamu pale kwa wakati huo.

Cate alifichua walipokuwa wanajuana uhusiano wao  haukuwa mzuri  vile kwani Karanja hakuwa anapendezwa na mienendo yake.

"Tulikutana baadae. Cha kushangaza zaidi ni kuwa hatuwahi pendana.Alidhani nilikuwa 'too much'. Alijua niko na talanta lakini alikuwa ananishangaa sana. Asubuhi tungeenda na binamu yangu (Tina) tukiwa na hangovers, hatuna mistari na ni yeye anaelekeza filamu anashangaa shida yetu ni nini" Cate alieleza.

Mwigizaji huyo alisema kwa wakati ule Karanja hangewahi amini kuwa siku moja wangekuwa mume na mke.

Alisema baada ya kujuana kwa muda mumewe alianza kumuona kama mtu mwenye maono na wakaanza kushauriana kuhusu masuala mbalimbali.

"Alikuwa mwelekezaji filamu wangu. Alianza kuona nilikuwa na maono, ni vile tu ni kachizi lakini ako na maono. Ningeendea ushauri kwake sana kwa kuwa alikuwa director wangu. Alianza kunisaidia kuweka brand yangu pamoja, hapo tu tukishauriana ndio hivo, nami nikajipata nimeshaurika na harusi ikapangwa" Cate alisimulia.

Cate alisema walichumbiana kwa kipindi cha takriban miaka minne kabla ya kupiga hatua ya kufunga pingu za maisha.

Alifichua kuwa yeye ndiye alimshinikiza mumewe wafunge ndoa kwa kuhofia asije akaachwa siku moja.

Wawili hao wamekuwa pamoja kwa kipindi cha takriban miaka  saba na wamebarikiwa na mtoto mmoja pamoja ambaye ana umri wa miaka saba.