"Nimemsababishia aibu na uchungu mwingi!" Akothee amsherehekea mama yake kwa kujivunia kuhusishwa naye

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo amekiri kwamba mtindo wake wa maisha umewahi kusababishia mama yake aibu kubwa miongoni mwa wazazi wengine wa rika lake.

•Amefichua kwamba mama yake hakuwa na amani wakati alikuwa anaugua na ameeleza  angetamani kumuona akiwa na furaha siku zote za maisha yake.

Akothee pamoja na mama yake Bi Monica Kokeyo
Akothee pamoja na mama yake Bi Monica Kokeyo
Image: HISANI

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri nchini Esther Akoth almaarufu kama Akothee amemsherehekea mama yake mzazi kwa kusimama naye licha ya aibu nyingi na masikitiko ambayo amewahi kumsababishia maishani.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mwanamuziki huyo amekiri kwamba mtindo wake wa maisha umewahi kusababishia mama yake aibu kubwa miongoni mwa wazazi wengine wa rika lake.

Mama huyo wa watoto watano hata hivyo ameweka wazi kwamba licha ya yote, mama yake angali anajivunia sana kuhusihwa naye.

"Ikiwa kuna mwanamke ambaye anajivunia mimi ni mama yangu! ! Baada ya kumvunja moyo na aibu zote nilizomsababishia miongoni mwa marafiki zake wa umri! Wakati wenzake wote walikuwa na watoto wenye nidhamu, wasichana walioelimika, walioolewa! Wake ilikuwa amepewa talaka, anauza sabuni! asiye  na matumaini, asiye  na kazi, asiye wa maana, asiye na ndoto na watoto mwenye watoto wengi. Nimemsababishia huyu mwanamke aibu na uchungu sana!" Akothee ameandika.

Msanii huyo amesema licha ya yote yaliyofanyika mama yake ameendelea kusherehekea maendeleo yake katika maisha na amekuwa akimuombea hasa alipokuwa mgonjwa.

Amefichua kwamba mama yake hakuwa na amani wakati alikuwa anaugua na ameeleza  angetamani kumuona akiwa na furaha siku zote za maisha yake.

"Mama yangu amekuwa na wasiwasi mwingi tangu nilipougua! Ameniombea. Mama yangu alilazimika kujifunza jinsi ya kutumia WhatsApp Video kwenye simu ili kuniona. Siku alipopiga simu na kunikuta bila kifaa cha kushikilia shingo ilibadilisha maisha yake! Aliniambia siku iliyofuata, alikuwa na usingizi mzito kwa mara ya kwanza tangu Oktoba. Nataka tu awe na raha!" Akothee amesema.

Akothee ni miongoni mwa wasanii waliozingirwa na  utata na drama nyingi za maisha katika taaluma zao.