"Utapendwa milele" Kambua aadhimisha mwaka mmoja tangu mwanawe afariki kwa njia maalum

Muhtasari

•Kambua alifanya sherehe ndogo ndani ya nyumba kwa ajili ya marehemu mwanawe na kuashiria hafla hiyo kwa maua na keki yenye maandishi 'For Malachi'.

•Alisema  anaamini kwamba mwanawe yuko mahali salama peponi ambako anaendelea kulindwa vizuri  hadi watakapokutana tena.

Mwanamuziki Kambua
Mwanamuziki Kambua
Image: Hisani

Katika kipindi cha siku tatu ambacho kimepita, mwanamuziki wa nyimbo za injili Kambua Manundu amekuwa akiadhimisha mwaka mmoja tangu mtoto wake Malachi Manundu aage dunia.

Mtangazaji huyo wa zamani wa  Citizen TV aliadhimisha mwaka mmoja tangu kumpungia mwanawe mkono wa buriani kwa njia ya kipekee.

Kambua alifanya sherehe ndogo ndani ya nyumba kwa ajili ya marehemu mwanawe na kuashiria hafla hiyo kwa maua na keki yenye maandishi 'For Malachi'.

Heri ya siku ya kuadhimishwa mwaka mmoja mbinguni Malachi wangu wa thamani . Tungependa kukukumbatia leo, lakini najua Yesu na malaika wamekufunika kwa upendo mwingi na hiyo inatupa amani. Unapendwa milele " Kambua alimsherehekea mwanawe kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Kambua alimshukuru Mola kwa kumpa zawadi ya mtoto na kusema kuwa ingawa mwanawe alifariki , bado anaamini kwamba yuko mahali salama peponi ambako anaendelea kulindwa vizuri  hadi watakapokutana tena.

Mwamuziki huyo vilevile amewatia moyo wazazi kama yeye ambao wamefiwa na watoto wao huku akiwaarifu kwamba Mungu ataendelea kuwapa nguvu maadamu wasalie waaminifu ndani yake.

Najua maumivu. Najua uchungu huo. Najua uzito uliopo. Lakini pia najua kuwa uchungu hupungua na giza hupita. Najua ukimruhusu Mungu hutatembea peke yako. Atakuwa pale kwa ajili yako. Kukukumbatia, kukufuta machozi, kukuinua.. Imepita mwaka mmoja tangu Malach aage na nimepitia kile ninachoweza kufupisha tu kama Shalom- amani; ukamilifu wa Mungu" Alisema.

.Mwanamuziki huyo ambaye amekuwa akitumbuiza kwa miaka mingi alimpoteza mtoto wake wa pili mnamo mwezi Februari mwaka uliopita.