Akothee afunguka jinsi alivyohangaika kutafutia bintiye shule baada ya kususia ambazo wanafunzi walinyolewa

Muhtasari

•Akothee amesema  kuwa bintiye alikataa katakata kujiunga na shule yoyote ambapo wanafunzi walilazimishwa wanyoe  nywele zao.

•Nywele ndefu za Rue Baby zilizua hali ya  kutoelewana vizuri kati yake na nyanyake ambaye alisisitiza watu waweke nywele zao zikiwa fupi,

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali Esther Akoth almaarufu kama Akothee amefichua kuwa binti yake wa pili Rue Baby hakutaka kupitishwa wembe kichwani kamwe katika enzi zake za shule.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee amesema  kuwa bintiye alikataa katakata kujiunga na shule yoyote ambapo wanafunzi walilazimishwa wanyoe  nywele zao.

Mama huyo wa watoto watano amefichua kuwa wakati Rue Baby alikuwa anajiunga na shule ya pili walilazimika kutafuta shule ambayo ingemruhusu ahifadhi nywele zake ambazo zilikuwa ndefu kwa wakati huo.

"Ilibidi tutafute shule ambayo ingemruhusu aweke nywele zake ndefu. Ililazimu tusafiri hadi Nyabohanse" Akothee alisema.

Nywele ndefu za Rue Baby zilizua hali ya  kutoelewana vizuri kati yake na nyanyake ambaye alisisitiza watu waweke nywele zao zikiwa fupi, Akothee amefichua.

Mwanamitindo huyo mwenye umri wa miaka 24 hata hivyo kwa sasa  amebadili mtindo wake wa maisha kwani siku hizi anapendelea kuweka nywele zake zikiwa fupi.

"Kwa sababu hizi Rue Baby alichukia kuenda ushago. Sasa 2022, Nani anafaa kuomba mwingine msamaha. Mamangu anafaa amuombe Rue ama ni Rue anafaa kuomba mamangu? Jitihada zangu za kukimbia ili nisiumize hisia zake kwa kukata nywele zake lazima zirudi" Akothee amesema.

Miaka kadhaa imepita tangu Rue Baby aweke nywele refu. Wengi wanamjua kuwa na nywele fupi kwa kuwa umaarufu wake mkubwa ulikuja akiwa na nywele fupi.