Kingwendu atazamia kuwapatanisha Diamond Platinumz na Harmonize

Muhtasari

•Kingwendu amesisistiza kuwa bado anawasaka mastaa hao wawili katika juhudi za kuleta amani kati yao.

•Alisema  mikwaruzano mingi inayoshuhudiwa katika tasnia ya muziki imetokana na ukosefu wa heshima miongoni mwa wasanii.

Diamond Platnumz, Mzee Kingwendu, Harmonize
Diamond Platnumz, Mzee Kingwendu, Harmonize
Image: HISANI

Mchekeshaji na mwigizaji mashuhuri kutoka Bongo Rashidi Mwinshehe almaarufu Kingwendu amesisitizia mpango wake wa kupatanisha wababe wawili wa muziki wanaoaminika kuwa na ugomvi, Diamond Platnumz na Harmonize.

Akiwa kwenye mahojiano na Top Level Tz, Kingwendu alisisistiza kuwa bado anawasaka mastaa hao wawili katika juhudi za kuleta amani kati yao.

Kingwendu alikubali kuwa ni jambo kawaida watu walio kwenye jukwaa moja kuzozana ila akawasihi wanamuziki wote kukuza upendo zaidi ya uhasama.

'Tutangulizeni upendo na amani katika nchi yetu. Sisi wenyewe tupendane na tutaishi kama amani.Hii kutishiana, kuitana mchawi hatutafika popote. Hii tasnia ya muziki itakuwa haina amani," Kingwendu alisema.

Mwigizaji huyo alisema  mikwaruzano mingi inayoshuhudiwa katika tasnia ya muziki imetokana na ukosefu wa heshima miongoni mwa wasanii.

Kingwendu alisema angependa sana Diamond  na Harmonize waache chuki na waweze kuelewana 

"Waishi kama Watanzania tunavyoishi kwa amani na upendo. Kusema samahani ni kitu kidogo na kikubwa sana. Waseme yaishe waendelee na maisha yao, virahisi tu," Kingwendu alisema.

Mchekeshaji huyo mkongwe pia  alisema kuwa angependa kufanya collabo na mastaa hayo ila kufikia sasa hajaweza kupatana nao.