Huwa nakula ugali kila siku, vyakula vingine ni glucose!- Charles Odongo 'Ugali man' adai

Muhtasari

•Odongo alieleza kuwa chakula hicho ambacho sana sana huhusishwa na jamii ya Waluhya humsaidia sana katika ujenzi wa mwili.

•Odongo alidai kuwa hakutarajia video ambayo ilimletea umaarufu mkubwa ingevuma sana jinsi ilivyovuma.

Image: FACEBOOK// CHARLES ODONGO UGALI MAN

Mtaalamu wa mazoezi Charles Odongo almaarufu Ugali Man amekiri upendo wake mkubwa wa chakula aina ya Ugali.

Akiwa kwenye mahojiano na Tuko Extra, Odongo alifichua kuwa ugali ni chaguo lake la kila siku la chakula.

Odongo alieleza kuwa chakula hicho ambacho sana sana huhusishwa na jamii ya Waluhya humsaidia sana katika ujenzi wa mwili.

"Napenda ugali. Mimi hula ugali kila siku, Januari hadi Desemba hakuna chakula kingine. Vyakula hivyo vingine ni glucose, mchele ni glucose ya kulambwa na hutasikia kitu.  Ukila ugali unaweza stahimili muda mrefu bila kuhisi njaa kwa kuwa inashika tumbo vizuri," Odongo alisema.

Baba huyo wa watoto watatu alifichua kwamba huwa anabadilisha tu kitoweo cha kuambatana na chakula hicho akipendacho.

Alisema kuwa anajivunia jina 'Ugali man' ambalo alibandikwa mwaka jana baada ya video iliyoonyesha akila ugali kwa mtindo wa kipekee kusambazwa mitandaoni.

"Nakubali jina hilo kwa kuwa napenda ugali. Mimi ni ugali man," Alisema.

Mtaalamu huyo wa mazoezi alidai kuwa hakutarajia video ambayo ilimletea umaarufu mkubwa ingevuma sana jinsi ilivyovuma.

Alisema alirekodi video hiyo kutumia simu yake akikusudia kutumbuiza marafiki wake wachache.