"Tumebarikiwa kuwa na wewe" Njugush amsherehekea mkewe kwa ujumbe maalum

Muhtasari

•Njugush amemtaja mkewe kama mama bora  kwa mtoto wao Tugi na kusema kuwa yeye ni baraka kubwa katika maisha yao.

•Njugush ameweka wazi kuwa ameridhika na malezi mazuri ambayo mkewe amempatia mtoto wao.

Image: INSTAGRAM// CELESTINE NDINDA

Huku dunia ikiadhimisha siku ya kina mama, mchekeshaji Timothy Kimani almaarufu Blessed Njugusha amemsherehekea mke wake Celestine Ndinda.

Njugush amemtaja mkewe kama mama bora  kwa mtoto wao Tugi na kusema kuwa yeye ni baraka kubwa katika maisha yao.

"Siku maalum ya akina mama WaTugi. Unatutunza sote bila kulalamika. Ni mengi uliyoyabeba kwenye mabega yako lakini haulalamiki. Hakika tumebarikiwa kuwa na wewe mwenye moyo mzuri. Tugi anajua ana Mama bora,juzi alisema nilimchagulia Mama mpoa. Nafurahi kuwa ni wewe, Singelitaka kwa njia nyingine yoyote," Njugush amemwandikia mkewe kupitia Instagram.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha ya kumbukumbu ya Ndinda akiwa amesinzia kwenye kochi huku akiwa amemkumbatia mtoto wao Tugi mikononi.

Mchekeshaji huyo ameweka wazi kuwa ameridhika na malezi mazuri ambayo mkewe amempatia mtoto wao.

"Siamini tuko hapa. Shukran kwa kusaidia sana katika hali zote. Asante kwa kumpenda tu mama yangu, inamaanisha kila kitu kwangu. Asante kwa kupalilia upendo na maisha .Tunakupenda Mama T². Neema zaidi na upendeleo, maisha zaidi na furaha," Njugush aliendelea kusema.

Ndinda kwa upande wake amemshukuru sana mumewe kwa ujumbe huo mtamu ambao amemwandikia.

Njugush na Ndinda walifunga ndoa mwaka wa 2016 baada ya kukutana na kujitosa kwenye mahusiano wakiwa katika chuo kikuu.

Hivi majuzi Ndinda alifichua kuwa mumewe hakuwahi kumtongoza katika juhudi za kuteka moyo wake. Alisema mumewe alikuwa rafiki wake wa karibu kabla hawajajitosa kwenye mahusiano.

"Tim hakuwahi kunikatia. Alikuwa rafiki mzuri. Hakuwahi niitisha numba. Ni kama alikuwa anataka msichana mwingine. Kuna beshte yangu ambaye walikuwa na kitu naye. Ni kama walikuwa na kitu kilichokuwepo. Siku moja tukitoka mjini simu ya rafiki yangu ikazima, akaomba simu yangu ili ampigie Tim. Hivo ndo alipata namba yangu," Ndinda alisema akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz.

Alisema toka wakati huo walianza kujuliana hali mara kwa mara na kadri walivyoendelea kuzungumza urafiki wao ukaendelea kunoga zaidi.

Wanandoa hao wawili wanatarajia mtoto wao wa pili hivi karibuni.