"Hakuwahi kunikatia" Wakavinye afunguka jinsi alivyokutana na mumewe Njugush

Muhtasari

•Ndinda alifichua kuwa walijuana kupitia rafiki yake ambaye Njugush alikuwa anamezea mate kwa wakati huo.

•Ndinda alifichua kuwa wakati walikuja kujuana na mumuwe tayari wote wawili walikuwa kwenye mahusiano mengine

Image: INSTAGRAM// NJUGUSH

Mwigizaji Celestine Ndinda almaarufu Wakavinye amefichua kuwa mumewe Njugush hakuwahi kumtongoza katika juhudi za kuteka moyo wake.

Akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz, Ndinda alisema mumewe alikuwa rafiki wake wa karibu kabla hawajajitosa kwenye mahusiano.

Alifichua kuwa walijuana kupitia rafiki yake ambaye Njugush alikuwa anamezea mate kwa wakati huo.

"Tim hakuwahi kunikatia. Alikuwa rafiki mzuri. Hakuwahi niitisha numba. Ni kama alikuwa anataka msichana mwingine. Kuna beshte yangu ambaye walikuwa na kitu naye. Ni kama walikuwa na kitu kilichokuwepo. Siku moja tukitoka mjini simu ya rafiki yangu ikazima, akaomba simu yangu ili ampigie Tim. Hivo ndo alipata namba yangu," Ndinda alisimulia.

Alisema toka wakati huo walianza kujuliana hali mara kwa mara na kadri walivyoendelea kuzungumza urafiki wao ukaendelea kunoga zaidi.

"Tulikuwa marafiki wazuri. Kusema kweli mimi sikuwa naona kitu. Alikuwa mtu mzuri na bado yeye ni mzuri," Alisema.

Ndinda alifichua kuwa wakati walianza kujuana na mumuwe tayari wote wawili walikuwa kwenye mahusiano mengine. Alisema walianza safari ya kuchumbiana baada ya mahusiano yao kugonga mwamba.

Mama huyo wa mtoto mmoja alifichua kuwa baba ya Njugush pia alichangia sana katika kufanikisha ndoa yao.

"Baba yake alimwambia 'huyu msichana umekaa naye sana, umemleta nyumbani na tumemuona sana unapanga vipi?'. Abel Mutua pia akamwambia akishakuwa staa itakuwa ngumu kupata mtu," Alisema.

Wawili hao walifunga ndoa mwaka wa 2016 baada ya kukutana na kujitosa kwenye mahusiano wakiwa katika chuo kikuu.