Kijana aliyedukua akaunti ya Kabarak University avunja kimya, adai 68,000 kuirejesha

Mwanafunzi huyo alieleza kwamba alikuwa akijifurahisha tu alipodukua akaunti hiyo na akaomba msamaha kwa hilo.

Muhtasari

•Ukurasa huo ulidukuliwa siku chache zilizopita na kijana kutoka Indonesia ambaye amekuwa akichapisha vitu vyake ikiwemo picha zake.

• "Sitarudisha akaunti hii, lakini ninawapa changamoto nyote kudai tena akaunti hii mara moja," alisema.

amedai Ksh 68,000 kuirejesha
Kijana aliyedukua akaunti ya Facebook ya Kabarak University amedai Ksh 68,000 kuirejesha
Image: HISANI

Mwanafunzi kijana wa kigeni aliyedukua ukurasa wa mtandao wa Facebook wa Chuo Kikuu cha Kabarak ameweka wazi kuwa hana mpango wa kurejesha usimamizi wake kwa  taasisi hiyo ya  masomo ya juu ya Kenya.

Ukurasa wa Kabarak University ulioidhinishwa , wenye wafuasi zaidi ya elfu arubaini ulidukuliwa siku chache zilizopita na kijana mwenye asili ya Asia ambaye amekuwa akichapisha vitu vyake ikiwemo picha zake.

Kijana huyo ambaye bado hajatambulishwa alikuwa akipost kwa lugha ya kigeni hadi Jumamosi jioni alipoamua kuwahutubia Wakenya kwa lugha watakayoelewa, Kiingereza na kuwafafanulia kuhusu kitendo chake.

Kwa ujasiri, alieleza wazi kwamba alikuwa akijifurahisha tu alipodukua akaunti hiyo na akaomba msamaha kwa hilo. Aliendelea kutoa changamoto kwa taasisi hiyo  kujaribu kurejesha akaunti hiyo  kama wanaweza.

"Habari zenu, hapa naomba tu nifafanue kuhusu akaunti hii iliyodukuliwa, kusema kweli nilikuwa najiburudisha tu msichukulie kwa uzito machapisho ninayochapisha, kwa mara nyingine tena samahani," alisema.

Aliongeza, "Sitarudisha akaunti hii, lakini ninawapa changamoto nyote kudai tena akaunti hii mara moja - (Salamu kutoka kwa mwanafunzi katika mojawapo ya shule za upili za IT za Jakarta.)

Mwanafunzi huyo wa Indonesia hata alikuwa mkarimu zaidi kupea taasisi hiyo chaguo jingine la kumlipa Ksh 68,000 ili kuwarejeshea akaunti.

"Pia nina chaguo lingine, nipeeni tu 500$ (68,000) na nitarudisha ukurasa huu, ofa ni nafuu kwa chuo kikuu kikubwa," alisema.

Taasisi hiyo  ya elimu ya juu iliyo katika kaunti ya Baringo hata hivyo  bado haijajibu madai ya mdukuzi huyo.

Siku ya Ijumaa, Chuo Kikuu cha Kabarak kilitoa taarifa kuthibitisha udukuzi wa akaunti yao ya mtandao wa  Facebook.

"Tunataka kuwahakikishia washikadau wote na umma kwa ujumla kwamba tunachukua hatua zote zinazohitajika kurejesha udhibiti wa ukurasa wetu wa Facebook na kuzuia ufikiaji wowote ambao haujaidhinishwa," shule hiyo alisema katika taarifa iliyotiwa saini na Makamu Mkuu wa Chuo, Henry .K. Kiplangat.

Taasisi hiyo ilikiri kuwa udukuzi huo ulisababisha fujo ikibainisha kuwa watazuia hilo kutokea katika siku zijazo.