Mwimbaji Otile Brown amthamini marehemu nyanyake kwa pambo la thamani

Pambo hilo lililotengenezwa kwa almasi linakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni moja.

Muhtasari

•Otile alionyesha pambo hilo la thamani linalometameta na lililounganishwa kwenye mkufu kisha kuwashukuru wabunifu waliomtengenezea.

•Marehemu Bi Elizabeth Onyango alihusika sana katika kumlea Otile Brown hasa baada ya wazazi wake kuaga dunia akiwa mdogo. 

katika picha ya maktaba
Otile Brown na Marehemu nyanya yake katika picha ya maktaba
Image: HISANI

Mwanamuziki mashuhuri wa Kenya Jacob Obunga almaarufu Otile Brown ameonyesha upendo mkubwa kwa marehemu nyanya yake, Elizabeth Onyango kwa kutengenezewa pambo maalum la almasi lenye sura yake.

Siku ya Ijumaa, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30, kwa fahari kubwa alionyesha pambo hilo la thamani linalometameta na lililounganishwa kwenye mkufu kisha kuwashukuru wabunifu waliomtengenezea.

"Shukran Elizabeth Onyango," maelezo kwenye pambo hilo yalisomeka.

Mwanamuziki huyo mwenye kipaji kinachoshabikiwa na wengi kote duniani aliendelea kumtakia marehemu nyanyake mapumziko ya amani na kumhakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

"Marehemu bibi yangu Elizabeth akiwa amezungukwa na almasi. Asante Ice Box. Nakupenda. Pumzika kwa amani," alisema.

Pambo hilo lililotengenezwa kwa Almasi linakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni moja.

Marehemu Bi Elizabeth Onyango alihusika sana katika kumlea Otile Brown hasa baada ya wazazi wake kuaga dunia akiwa mdogo. Brown alizaliwa na kulelewa katika kaunti ya Mombasa lakini kwa bahati mbaya wazazi wake wote wawili walifariki akiwa bado mdogo ambapo baadaye alichukuliwa na wanafamilia.

Wakati akihojiwa na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Radio Jambo Julai mwaka jana, mwimbaji huyo mahiri alizungumza kuhusu maisha yake magumu ya utotoni baada ya wazazi wake wote kuaga.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30 alifichua kwamba wazazi wote wawili walifariki akiwa na umri mdogo.

“Mama alifariki, Baba alifariki. Sikulelewa na baba, slifariki nikiwa mchanga. Mama alifariki nikiwa na miaka 12. Nililelewa na mamangu mdogo,” Alisema.

Brown alisema yeye ni mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watano. Alifichua kuwa yeye na ndugu zake walikua katika hali ngumu baada ya wazazi wote wawili kufariki.

Pia alieleza kuwa shangazi yake na majirani ndio waliofanikisha masomo yake hadi hatua ya kidato cha nne.

Wakati huo huo, alifichua kwamba alificha utambulisho wake wa kabila kwa muda mrefu huku akiweka wazi kuwa wazazi wake wote wawili walitokea jamii ya Luo.

Otile hata hivyo hakujitambulisha na jamii hiyo kwa kuwa alikua miongoni mwa Waswahili na alihofia kutengwa kwa misingi ya kikabila.

“Mimi nimezaliwa Mombasa kwenye jamii ya Waswahili. Kama unavyojua kitambo kulikuwa na ukabila na mimi sikutaka kipaji changu kipunguzwe katika eneo fulani,” Otile alisema.

Mwimbaji huyo pia alisema hakutaka kujihusisha na jamii yake kutokana na sifa ya majigambo wanayohusishwa nayo. Alidai kuwa utambulisho wake wa kabila ulijulikana baadaye maishani baada ya kufanya shughuli ya Mpesa ambapo mtu asiyejua alichukua hatua ya kutangaza maelezo yake rasmi