Diamond? Harmonize atangaza wimbo na msanii aliyekuwa akiombeana mabaya naye

“Ninacheka sanaa nikiwaza vipindi tulivyokuwa hata tunaombeana mabaya kabla tujue kuna Mungu na kuna upendo," Harmonize alisema.

Muhtasari

•Konde Boy alidokeza zaidi kuwa hapo awali alikuwa na uhusiano mbaya na msanii huyo, hadi wakati walipojua kuna Mungu na kuna upendo.

•Mashabiki wengi wameamini kuwa huenda ni bosi wake wa zamani, Diamond Platnumz, au mwenzake wa zamani, Rayvanny.

katika picha ya maktaba.
Harmonize na Diamond katika picha ya maktaba.
Image: HISANI

Staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amezua tetesi baada ya kudokeza kuhusu kuachia wimbo mpya ambao amefanya na msanii wa kiume ambaye hajawahi kufanya naye kolabo kwa miaka ya hivi karibuni.

Katika chapisho la Jumanne jioni, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alidokeza kuwa ataachia wimbo na ‘kaka’ yake ambaye hajakuwa naye studioni kwa zaidi ya miaka minne iliyopita.

Konde Boy alidokeza zaidi kuwa hapo awali alikuwa na uhusiano mbaya na msanii huyo, hadi wakati walipojua kuna Mungu na kuna upendo.

"Sijawahi kuwa naye studio kwa zaidi ya miaka minne. LOL, inachekesha kwamba tulikuwa tukingojea hii. Hit nyingine kwenye game Ijumaa hii na kaka yangu,” Harmonize alisema kupitia Instastories yake.

Aliongeza, “Ninacheka sanaa nikiwaza vipindi tulivyokuwa hata tunaombeana mabaya kabla tujue kuna Mungu na kuna upendo.”

Bosi huyo wa lebo ya Konde Music Worldwide alitaka mashabiki wake wamkisie msanii ambaye ameingia naye katika studio.

Kulingana na maelezo ya msanii huyo ambayo Konde Boy ameyatoa, mashabiki wengi wameonekana kudhani kuwa huenda ni bosi wake wa zamani wa WCB, Diamond Platnumz, au mwenzake wa zamani katika lebo hiyo, Rayvanny.

Wimbo wa mwisho ambao bosi huyo wa Kondegang alifanya na Diamond ulikuwa ‘Kainama’ uliotolewa Machi 2019. Wasanii hao wawili wakubwa kutoka Tanzania pia walimshirikisha nyota wa Nigeria Burna Boy katika wimbo huo. Hapo awali walikuwa wametoa nyimbo kadhaa pamoja zikiwemo ‘Kwangwaru’, ‘Bado’ na ‘Zilizopendwa.’

Baadaye Harmonize aliondoka Wasafi mwaka wa 2019 na kisha akaenda kuunda lebo yake ya muziki, Konde Music Worldwide.

Harmonize alianza kupata umaarufu baada ya kukutana na Diamond Platnumz na kusainiwa katika WCB Wasafi mwaka 2015. Uhusiano kati ya mastaa hao wawili wa bongo fleva hata hivyo uliharibika mwaka wa 2019 ambapo Harmonize allichukua hatua ya kuondoka katika lebo hiyo na kuwa msanii huru.

Mapema mwaka jana, bosi huyo wa Konde Music Worwide aliripotiwa kupiga hatua ya kutafuta huduma za mawakili kumsaidia kuishtaki lebo ya WCB inayomilikiwa na  Diamond kwa madai ya kunufaika na jasho lake.

Konde Boy alisema WCB imeshirikiana na wasambazaji wa muziki, Mziiki, kuchukua fedha zinazotokana na muziki wake akidai zilikuwa zinaenda kwenye akaunti ya lebo hiyo badala ya yake licha ya mkataba wake kusitishwa.

“Wasafi na Mziiki wameshirikiana kunichafua ila sijawakosea. Imekuwa kibarua kubwa kupata kile ambacho ni changu kutoka kwao ili niweze kulisha familia yangu kama wanavyofanya na familia zao," alisema mwezi Machi.

"Kwa nini waninyime kupata haki yangu ya Haki Miliki (IP) huku wakiendelea kukusanya pesa kutoka kwa IPs zangu kwa niaba yangu,” alihoji.

Wakati huo, wimbaji huyo wa kibao  'Single Again' alisema anakamilisha mipango na mawakili wake ili kupeleka kesi hiyo mahakamani hivi karibuni.

Pia alitoa wito kwa Waziri Msaidizi mpya wa Utamaduni na Sanaa, rapa Mwana FA, kumsaidia kutatua mzozo huo.

"Ninamtegemea atanisaidia kwa sababu nimeshindwa kukusanya mirabaha yangu ya muziki kwa miaka mitatu,” alisema.