Akothee afichua jina kamili la mumewe, siku ambayo angejifungua mimba aliyopoteza

Mama huyo wa watoto watano alimhakikishia mumewe Omosh kuwa watapata mtoto pamoja hivi karibuni.

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano aliweka wazi kuwa hana majuto yoyote ya kufunga pingu za maisha na mzungu huyo.

•Licha ya kupoteza ujauzito wake miezi kadhaa iliyopita, alimhakikishia Omosh kwamba watapata mtoto pamoja hivi karibuni.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mume wa mwimbaji na mjasiriamali Akothee, Denis Shweizer almaarufu Omosh anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Huku akimsherehekea kwenye Instagram, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alisema ana bahati kuwa mke wake.

"Denis Eduard Schweizer Omondi wa 7 amekuwa mwanaume wa aina yangu. Siku zote nimekuwa nikitaka mtu ambaye anaweza kuchafua mikono yake, mwenye nguvu, kichaa, mwenye upendo, mwenye kuudhi na zaidi ya yote mwenye kujali," Akothee aliandika Jumatano na kuambatanisha na picha za mumewe.

Aliongeza, "Siku zote nimekuwa nikitaka rafiki ndani ya mahusiano, mtu mwenye nia wazi na mwenye kuelewa kwa hali ya juu kwa sababu AKOTHEE ni taasisi yenye matawi mbalimbali ya wazimu. Mwanaume mwenye wazimu kidogo tu ndiye anayeweza kumuelewa Esther, Esther si mwanamke wa wavulana, anavutia wanaume na kuwatisha wavulana, ndio maana AKOTHEE NDIYE KIPIMO CHA MAFANIKIO."

Mama huyo wa watoto watano aliweka wazi kuwa hana majuto yoyote ya kufunga pingu za maisha na mzungu huyo.

“Nilikuchagua wewe na huyo ni mume wangu hapo,” alisema.

Akothee pia alitumia fursa hiyo kumkumbuka ambaye angekuwa mtoto wao wa kwanza pamoja ambaye angezaliwa miezi miwili ijayo.

Licha ya kupoteza ujauzito wake miezi kadhaa iliyopita, alimhakikishia Omosh kuwa watapata mtoto pamoja hivi karibuni.

"Nina furaha sana kuanza safari mpya. Mister Omosh ungeweza kuwa baba tarehe 22 Julai 2023 lakini ya ulimwengu hutokea na tutakuwa wazazi tena hivi karibuni mpenzi wangu. Niruhusu nikutakie kheri njema. Kheri ya siku ya kuzaliwa mfalme wa umalkia wangu. Heri ya siku ya kuzaliwa  Omondi wa saba," alisema.

Takriban wiki mbili zilizopita, mwanamuziki huyo alidokeza  kwamba ameanza maandalizi ya safari yake ya ujauzito.

Mama huyo wa watoto watano kupitia ukurasa wake wa Instagram alionyesha pakiti ya dawa aina ya Pregnacare Plus Omega-3 ambayo kwa kawaida hutumiwa na wanawake wakati wa safari ya ujauzito.

"Yoooo safari inaanza sasa NDILAS," Akothee alisema chini ya video fupi ya dawa hizo ambayo alichapisha.

Hii ilikuwa siku chache baada ya mwimbaji huyo kutangaza mpango wa kuchukua mapumziko kutoka kwa mitandao ya kijamii.

Katika taarifa yake ya mwezi jana, mama huyo wa watoto watano alidokeza kuwa madhumuni ya mapumziko yake ya muda usiobainishwa yangekuwa kuangazia kuongeza mtoto mwingine na mume wake Omosh.

Aliwaomba mashabiki wake wamruhusu achukue mapumziko akisema anataka kupata mtoto wake wa sita hivi karibuni.

"Sasa nyie mnipe muda. Nitapumzika kutoka kwa kila mtu na kila kitu pamoja na mitandao ya kijamii. Mniruhusu nitafute mtoto wangu wa pili kutoka mwisho, kabla hatujazungumza mambo mengine.  Nataka kuwa mama mwaka huu," Akothee alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.