'Nimechoka kuwa mtumwa wenu!' Zari Hassan akatiza uhusiano na wanamitandao kufuatia uvumi kwamba amefunga ndoa

Muhtasari

•Zari ametangaza kwamba amekatiza uhusiano wake na mashabiki wake mitandaoni huku akieleza kwamba hatakubali kupatwa na msongo wa mawazo kwa sababu ya wanamitandao.

•Mzaliwa huyo wa Uganda na ambaye alikuwa mpenzi wa staa wa Bongo Diamond Platinumz ameapa kwamba kamwe hatawahi kueleza tena watu wasiojuana kuhusu jambo lolote linalohusiana na maisha yake.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasoshalaiti na mjasiriamali mashuhuri Zari Hassan amesema kuwa amechoka kueleza watu kuhusiana na maisha yake mitandaoni.

Mzaliwa huyo wa Uganda na ambaye alikuwa mpenzi wa staa wa Bongo Diamond Platinumz ameapa kwamba kamwe hatawahi kueleza tena watu wasiojuana kuhusu jambo lolote linalohusiana na maisha yake.

Kupitia ukurasa wake wa  Instagram, Zari amesema kwamba hataendelea kuwa mtumwa wa wanamitandao huku akiwashauri waamini kila fununu wanazosikia kumhusu.

"Kuwa mitandaoni kumefanya wengine wetu tuwe watumwa wenu. Hatuwezi fanya lolote bila kukosolewa na kuhukumiwa. Hatufahi kuwa hapa tunawaeleza tunachofanya, kwa nini tunakifanya na tunafanya na nani.Kutoka leo kwenda mbele kila unachoona mitandaoni amini tu unavyotaka kuamini. Sitaendelea kuwa mtumwa eti kwa sababu wa wanataka kujua kitu. Kwa kweli mimi nimechoka kueleza watu tusiofahamiana kuhusu maisha yangu. Amini unachoona na kusikia.Inachosha sana kuwa kueleza watu msiojuana kuhusu maisha yangu" Zari alisema.

Mama huyo wa watoto watano alisema kwamba hajalishwi na uvumi ambao unaenezwa dhidi yake mitandaoni.

Zari ametangaza kwamba amekatiza uhusiano wake na mashabiki wake mitandaoni huku akieleza kwamba hatakubali kupatwa na msongo wa mawazo kwa sababu ya wanamitandao.

"Mimi sitakubali kuathirika na msongo wa mawazo kwa sababu ya wanamitandao na wanachofikiria. Huu uhusiano na nyinyi umeisha kabisa. Acheni kunifuata kama hamjiskii" Zari alieleza.

Hapo awali mfanyibiashara huyo nchini Afrika Kusini alilazimika kueleza kuhusiana na picha zilizokuwa zinaenezwa mitandaoni ikidaiwa kwamba alikuwa amefunga pingu za maisha.

Zari alieleza kwamba picha hizo zilikuwa za video ya muziki ambao unatolewa hivi karibuni.

"Kuna picha ambazo zinaenea mitandaoni, tafadhali zipuuzilie. Hizo ni za wimbo wa injili wa mtumishi maarufu wa Mungu ambao unakuja, puuzilia kila kitu unachosoma mitandaoni" Zari alisema.