"Kajala alinifahamu vizuri zaidi" Harmonize amsifia aliyekuwa mpenzi wake Frida Kajala huku akiomba msamaha

Harmonize alikiri amewahi kuchumbia wanawake watatu pekee

Muhtasari

•Harmonize alimtambua mchumba huyo wake wa hivi karibuni kama mtu aliyemuonyesha mapenzi zaidi na kumuelewa vizuri huku akimuomba msamaha kwa mabaya aliyomfanyia.

•Alisema anajuta yote ambayo yalitokea kati yake na Kajala kuhusiana na bintiye huku akimsifia kama mama bora.

•Konde Boy alimtakia Kajala mafanikio mazuri maishani huku akisema anatumai siku moja urafiki wao utarejea.

Harmonize na Frida Kajala
Harmonize na Frida Kajala
Image: HISANI

Hivi majuzi mwanamuziki Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize  alizindua albamu yake ya pili 'High  School'.

Staa huyo wa Bongo alitumia ukurasa wake wa Instagram kufafanulia mashabiki wake maana ya nyimbo ishirini zilizo kwenye albamu yake mpya.

Harmonize alisema wimbo nambari saba katika albamu yake mpya 'Mtaje' ambao aliandikia aliyekuwa mpenzi wake Kajala Masanja ndio ulikuwa wa kihisia zaidi.

Alimtambua mchumba huyo wake wa hivi karibuni kama mtu aliyemuonyesha mapenzi zaidi na kumuelewa vizuri huku akimuomba msamaha kwa mabaya aliyomfanyia.

"Samahani kama nitaumiza yeyote. Kajala alinijua zaidi. Alikuwa anajua mimi ni mtu wa aina gani na napenda nini kwa wakati gani. Naamini alikuwa ananifahamu vizuri. Niamini, sitaki kuenda zaidi kueleza ilivyokuwa lakini nataka kuchukua fursa hii kama mwanaume kumuomba msamaha. Nahisi kilichofanyika ni mimi nilisababisha.Sipendezwi na kilichotokea kama mwanaume. Mimi ni mwanaume, lawama zote zije kwangu" Alisema Harmonize.

Konde Boy alisema hakuwahi kuwa na chuki yoyote kwa binti ya Kajala, Paula huku akidai alimpenda kama mtoto wake tu.

Alisema anajuta yote ambayo yalitokea kati yake na Kajala kuhusiana na bintiye huku akimsifia kama mama bora.

"Haijalishi nini, sikufaa kureacti vile. Nahisi vibaya sana. Naona niliingiza mtu kwenye matatizo, mambo ya kupelekana kwa polisi. Nimefanya aonekane sio mama bora. Ninachoamini na najua, Kajala alikuwa anajaribu sana kwa binti yake. Alijaribu sana kumfanya bintiye bora. Naamini yeye ni mzuri" Harmonize alisema.

Alisema anaamini kuwa kufikia sasa mama ya mpenzi wa Rayvanny tayari ameuguza maumivu na anaamini kwamba atasamehewa.

"Tulikuwa na hadithi nzuri ya mapenzi pamoja. Tulipendana sana na kila mtu anajua. Huwezi sema hatukupendana. Akiniambia kitu nilikuwa nafanya. Alinibadilisha. Alifanya mengi sana" Alisema.

Konde Boy alimtakia Kajala mafanikio mazuri maishani huku akisema anatumai siku moja urafiki wao utarejea.