Vera Sidika aapa kufanyiwa upasuaji mwingine wa matiti baada ya kuridhika na kupata watoto

Muhtasari

•Mama huyo wa binti mmoja amesema anatamani kupata matiti yenye umbo wa mviringo na ambayo yameinuliwa.

•Amesema kwamba binti yake amekuwa akifurahia maziwa kutoka kwa matiti yake tangu alipoionja kwa mara ya kwanza.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti mashuhuri Vera Sidika ameapa kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha umbo wa matiti yake punde baada ya kutosheka na kupata watoto.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa binti mmoja amesema anatamani kupata matiti yenye umbo wa mviringo na ambayo yameinuliwa.

Vera ambaye miaka michache iliyopita alifanyiwa upasuaji wa kuongeza ukubwa wa matiti yake pia ameweka wazi kwamba amekuwa akijivunia sana kumnyonyesha binti yake Asia Brown.

"Kunyonyesha haijawahi kunisumbua hata kidogo. Ninafanya hivyo kwa kujivunia na furaha nyingi. Mara tu baada ya kumaliza kupata watoto, hakika nitafanyiwa upasuaji wa  kubadilisha umbo wa matiti yawe ya kuvutia, ya mviringo na yaliyoinuka," Vera amesema.

Mwasoshalaiti huyo amesema kwamba binti yake amekuwa akifurahia maziwa kutoka kwa matiti yake tangu alipoionja kwa mara ya kwanza.

Vera ameeleza kuwa maziwa yake ndiyo yamemfanya binti yake kuonekana mnene miezi kadha tu baada ya kuzaliwa.

"Anajua tofauti kati ya maziwa ya unga na maziwa ya mama. Wakati ninaleta titi langu kwake angeweza kulishika... Hakuzaliwa akiwa mnene hivi, alikuwa mdogo kwa sababu alikuja wiki mbili kabla ya siku ya kuzaliwa. Yote ni kutokana na bidii yangu katika kunyonyesha," Vera amesema.

Vera alijifungua mtoto wake wa kwanza mnamo Oktoba 2021 akiwa na umri wa miaka 32.