Xtian Dela: Nimejitoa kinyang'anyiro cha ubunge Westlands

Muhtasari
  •  Dela ambaye mwaka wa 2021 aliweka wazi azma yake ya kutaka kuwa mbunge wa Westlands jijini Nairobi ameonekana kuchukua uamuzi wa kushtusha wengi wa wafuasi wake.
  •  Xtian Dela ambaye ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi Zaidi ya milioni moja ulizamishwa na  mamlaka husika, amewatupia wakenya lawama kwa masaibu hayo na ndio maana ametundika video hiyo kwenye ukurasda wa Telegram.
Xtian Dela
Xtian Dela
Image: Instagram

Aliyekuwa mwanahabari na mwanablogu Xtian Dela ametangaza kujitoa kabisa katika siasa. Dela ambaye mwaka wa 2021 aliweka wazi azma yake ya kutaka kuwa mbunge wa Westlands jijini Nairobi ameonekana kuchukua uamuzi wa kushtusha wengi wa wafuasi wake.

Katika mkanda wa video ambao Xtian Dela aliweka kwenye ukurasa wake wa Telegram Januari 27 usiku, Dela ameelezea kwamba uamuzi wake wa kujitoka katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Westands umesababishwa na masuala matatu ambayo anasikika akiyataja katika video hiyo yenye urefu wa takribani nusu saa hivi.

Baadhi ya masuala ambayo ameyaibua ni Wakenya kumtupia cheche za matusi na majungu kwenye mitandao huku akisema kuwa baadhi ya wakenya hao ni wale aliwasaidia wakati janga la Corona lilipobisha hodi nchini Kenya mapema mwaka 2020.

Mwanablogo huyo ameelezea kutamaushwa kwake na wakenya waliomfeli wakati alitangaza kuwania ubunge akidhani watalifurahia jambo hilo, ila majibu aliyoyapata ni matusi na masimango mitandaoni. Xtian Dela anasikika akisema,“wakenya hawako tayari kabisa kukaribisha mabadiliko maishani mwao. Wakenya bado hawajachoka na siasa za udanganyifu. Siku hizi, Wakenya hata hawawezi kujitokeza na kuandamana kwa minajili ya kusukuma mabadiliko, na ndio maana nimejitoa katika siasa kwa sababu ni mchezo mchafu.”

Suala la pili ambalo amesema limemsababishia kurudisha mpira kwa kipa ni kwamba hana pesa za kutumia katika misururu ya kampeni zake,

“Nimekosa pesa, nahitaji kima kama cha milioni 20 ama 30 ili kufanya siasa. Mimi si mjinga kusema kwamba nitatumia pesa zangu zote ambazo nimetia jitihada nyingi kuzitafuta kwa takribani miaka 15 ambayo nimekuwa nikijishughulisha na mambo mbali mbali kwenye mitandao.

Siwezi fanya kitu kama hicho. Mimi nikifikiria kuingia katika siasa nilidhani nitafuta dhana ya siasa za pesa kutoka vichwani mwa wakenya lakini kwa bahati mbaya nimeshindwa.” Alisema Dela.

Mwanablogu huyo aliweka mkanda huo wa video katika ukurasa wake wa Telegram na kusema kwamba imemchukua muda sana kujua jambo la kufanya kwani kwa muda mrefu tu amekuwa mhasiriwa wa matusi ya mitandao, jambo ambalo kidogo limpelekee kujitia kitanzi mwaka wa 2015, na pia mwaka 2021 alipotangaza kuwania ubunge Westalands, alipokea matusi kutoka kila pembe ya mitandao, suala ambalo lilimkatisha tamaa kwa wakenya kabisa.

Xtian Dela ambaye ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi Zaidi ya milioni moja ulizamishwa na  mamlaka husika, amewatupia wakenya lawama kwa masaibu hayo na ndio maana ametundika video hiyo kwenye ukurasda wa Telegram.