Dorea Chege adai kutishiwa maisha baada ya kujitosa kwenye siasa

Muhtasari

• Muigizaji maarufu Dorea Chege ameibua madai mapya kwamba amepokea arafa kadha wa kadha kutoka kwa watu wasiojulikana wanaomtishia kutokana na tangazo lake la kuwania uwakilishi wa kike Nairobi.

Dorea Chege
Image: Instagram

Muigizaji maarufu Dorea Chege ameibua madai mapya kwamba amepokea arafa kadha kutoka kwa watu wasiojulikana wanaomtishia kutokana na tangazo lake la kuwania kiti cha mwakilishi wa kike wa Nairobi.

Chege, ambaye alipata umaarufu kwa jina Magie alipokuwa akiigiza katika kipindi maarufu cha Maria kwenye runinga ya Citizen, juzi alitangaza azma yake kuingia katika siasa za kaunti ya Nairobi.

Katika video kwenye ukurasa wake wa Instagram, Chege amesema kwamba amepokea jumbe za kumtishia maisha tangu alipoweka wazi kuwania nafasi hiyo kama mgombea huru.

Dorea Chege
Image: Instagram

“Jina langu ni mheshimiwa Dorea Chege, na kama mnavyojua mimi ndiye ninawania kiti cha mwakilishi wa wanawake Nairobi. Sina furaha kabisa kwa sababu nimepokea arafa za simu kadha kutoka kwenu mnaonitishia" Dorea alisema.

Aliongeza kuwa ..."Acha niwambie kitu, siko tayari kuachilia azma yangu hiyo, na kitu kimoja mnafaa kujua, mimi si mtu muoga, huenda sina hizo pesa lakini acha niwambie kitu, tupatane kwa debe. Kura iongee!” aliteta Doreen.