Mnipe sifa kwa kufanya kutembea uchi kuwa kawaida- Akothee ajigamba

Muhtasari

•Akothee amesema kwamba wanawake wengi sasa wamezoea kuvaa mavazi madogo yasiyoficha uchi wote.

•Amesema anastahili sifa kwa kuwa aliteseka sana alipokuwa anapigania wanawake wasionekane kama wasio wa kawaida kwa kuonyesha uchi kidogo.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu kama Akothee amejivunia kufanya wanawake kutembea wakiwa nusu uchi kuonekana kama jambo la kawaida hapa nchini Kenya.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee amesema kwamba wanawake wengi sasa wamezoea kuvaa mavazi mafupi yasiyoficha uchi wao wote.

Mama huyo wa watoto watano amedai kuwa yeye ndiye aliyefanya wanawake kutoficha uchi wote isionekane kuwa suala kubwa kama ilivyokuwa miaka ya hapo awali.

"Nilifanya hali isiyo ya kawaida kuwa ya kawaida. Sasa mmegundua kuwa kila mwanamke anataka kuonyesha ngozi ndogo.  Mwili kidogo tu ndio inasumbua. Mnipe sifa NIPE ya kufanya kutembea uchi kuwa kawaida" Akothee alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 42 alikumbuka jinsi alivyokejeliwa na kutusiwa wakati alipojitosa kwenye tasnia ya muziki akiwa amevalia bikini.

Akothee amesema anastahili sifa kwa kuwa aliteseka sana alipokuwa anapigania wanawake wasionekane kama wasio wa kawaida kwa kuonyesha uchi kidogo.

"Nilisulubiwa, nikanyanyaswa kwa ajili yenu! Nilifanya jambo lisilo la kawaida kuwa la kawaida." Akothee alisema.

Kwa kipindi cha miaka mingi tangu alipopata umaarufu Akothee amekuwa akikosolewa sana kutokana na mtindo wake tatanishi wa maisha.