Valentino: Mwanamke amweka mumewe kwenye bango barabarani

Muhtasari

• Mtangazaji na mwekezaji mashuruhuri nchini Tanzania, Zamaradi Mketema amelipia bango la matangazo na kuweka picha ya mumewe kwenye barabara ambayo anasema mumewe ana mazoea ya kuitumia.

• Zamaradi alisema kwamba wana miaka mitano katika ndoa na sita tangu mahusiano yao kuanza

Mtangazaji na mwekezaji mashuruhuri nchini Tanzania, Zamaradi Mketema amekiuka mipaka na kuwapa changamoto wanawake wenza baada ya kutumia njia tofauti kabisa ambayo haijapata kutumika, kumuonesha mumewe mahaba na mapenzi msimu huu wa  siku kuu ya wapendanao - Valentino.

Zamaradi amelipia bango la matangazo na kuweka picha ya mumewe kwenye barabara ambayo anasema mumewe ana mazoea ya kuitumia.

Katika bango hilo kubwa, Zamaradi ameweka picha kubwa ya mumewe na kuifuatisha kwa maandishi "acha dunia ijue nakupenda kiasi gani, YOU ARE MY KING, happy Valentine’s day my love…… from your loving Wife"

Akihojiwa na mtangazaji wa shirika la habari la Clouds, Millard Ayo, mwanamke huyo amesema kwamba bango hilo aliliandaa kwa muda wa wiki mbili na kwamba amelilipia liwepo hapo barabarani kwa muda wa mwezi mzima.

"Hii ni barabara ambayo anapenda sana kupita yani kila siku lazima apite ndio maana nimeliweka pale," alisema Zamaradi

"Baada ya kuliweka nilimchukua mpaka pale amefurahi sana, tulipofika pale alicheka sana alafu akaingia kwenye gari machozi yakawa yanamtoka akaanza kulia akawa ameinama kwenye gari akasema kwahiyo Mke wangu umeamua kuniweka hapa juu…… amefurahi sana kwakweli” aliongeza mwanamke huyo katika mahojiano hayo ya simu.

Zamaradi alisema kwamba wana miaka mitano katika ndoa na sita tangu mahusiano yao kuanza na amesema nia yake kuu kumpakia mumewe kwenye mabango ya matangazo ya kibiashara ni kwa sababu ya upendo wake usiomithilika.

Mume wangu amekua ni Mtu flani ambae amenifanyia vitu vingi hakuna Mtu ambaye anaweza akajua ... amekua ni Mtu ambae ananipenda sana hata maneno hayawezi kutosha kumuelezea ni Mwanaume wa namna gani kwenye maisha yangu" amemalizia Zamaradi.” 

ama kweli yaani mapenzi mubashara yapo tena kwa sana. Wewe umefanyiwa nini cha mno na mpenzi wako siku hii ya Valentino?