'Nilimuweka kwenye bango na nikaachwa!' Eric Omondi afunguka kuhusu uchungu wa kuachwa na Chantal

Muhtasari

•Eric alisema alitumia pesa zake nyingi sana kudhihirisha mapenzi yake kwa malkia huyo mwenye asili ya Italia.

•Alifichua kuwa yuko katika harakati za kutafuta mke atakayeanzisha familia naye kwa kuwa miaka yake imeendelea kusonga.

Eric Omondi na Chantal Grazioli
Eric Omondi na Chantal Grazioli
Image: ERIC OMONDI SOCIAL

Mchekeshaji mashuhuri Eric Omondi amekiri kwamba aliumwa sana baada ya kutemwa na mpenziwe wa zamani Chantal Grazioli licha ya kumbubujikia mahaba tele.

Akiwa katika ziara yake nchini Tanzania, Eric alizungumza na waandishi wa habari na kukiri kuwa alianza kuogopa mapenzi baada ya kuachwa na Bi. Grazioli.

Eric alisema alitumia pesa zake nyingi sana kudhihirisha mapenzi yake kwa malkia huyo mwenye asili ya Italia na ndiposa aliachwa na uchungu mwingi moyoni baada ya mahusiano yao kugonga ukuta.

"Kuna muda nilishaweka mpenzi wangu kwenye bango. Niliweka bango mingi sana lakini bado nikaachwa. Ilikuwa ni uchungu sana maanake niifanya yote. Nilinunua gari, nikaweka bango na kufanya chochote" Eric alisema.

Mchekeshaji huyo alikiri kwamba huwa inauma sana kila anapokumbuka kuhusu mambo mazuri aliyomfanyia Bi Grazioli na bado mahusiano yao yakakosa kufua dafu.

"Nikikumbuka hiyo stori ya bango inaniuma sana moyoni. Ilinigharimu pesa nyingi. Niliweka pale kwa uwanja wa ndege. Kutoka siku hiyo nayaogopa sana mapenzi" Alisema.

Eric alidai kuwa kwa sasa hana mchumba wala mtoto yeyote.

Hata hivyo alifichua kuwa yuko katika harakati za kutafuta mke atakayeanzisha familia naye kwa kuwa miaka yake imeendelea kusonga.

"Natafuta mke. Nimekuwa nikitafuta mke kupitia Wife Material imeshindikana. Nahitimu miaka 40. Sina mtu, sina mtoto, sina bibi" Alisema

Matamshi hayo ya Eric hata hivyo yaliibua gumzo kuona kwamba wengi wanafahamu kuwa yeye ndiye baba mzazi wa mtoto wa Jacque Maribe.